Yatani awajibu wandani wa Ruto kuhusu salio la 93m kwa hazina ya kitaifa

Yatani ametaja madai ya viongozi wa Kenya Kwanza kama kutojua taratibu za mambo ya kifedha.

Muhtasari

• Baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza akiwemo Seneta wa Nandi Samson Cherargei walidai kwamba walipata Shilingi milioni 93 pekee katika Hazina.

• Yatani alisema serikali haikusanyi pesa,  kuzihifadhi pahali,  kwa muda wa mwezi kabla ya kuzisambaza baada ya mwezi au mwaka mmoja.


Waziri wa Fedha Ukur Yatani

Waziri wa Fedha Ukur Yatani ametaja madai ya viongozi wa Kenya Kwanza kwamba walipata shilingi milioni 93 pekee kwenye hazina ya kitaifa kama kutojua taratibu za mambo ya kifedha.

Yatani alisema serikali haikusanyi pesa,  kuzihifadhi pahali,  kwa muda wa mwezi kabla ya kuzisambaza baada ya mwezi au mwaka mmoja.

"Wakati mwingine tunabishana kwa kutojua. Kwa kweli sijui kama niihurumie hali hiyo kwa sababu kuna ujinga mwingi," Yatani alisema.

Baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza akiwemo Seneta wa Nandi Samson Cherargei walidai kwamba walipata Shilingi milioni 93 pekee katika Hazina.

Huku akisisitiza kuwa hilo linawezekana, Yatani alisema mapato yanayokusanywa na serikali yanatumika moja kwa moja.

"Tunaongeza mapato kila siku na tunafadhili serikali kila siku na kuna mahitaji yanayoshindana," aliongeza.

Waziri huyo aliyasema hayo siku ya  Alhamisi alipokuwa akiwahutubia maseneta  mjini Naivasha.

Alikuwa akizungumzia suala la kucheleweshwa kwa utoaji wa fedha kwa serikali za kaunti.

Waziri alisema baada ya kukusanya mapato ya kila siku au kila wiki, pesa hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ambapo mishahara ya wafanyikazi, mapato ya kaunti, Bunge, Mahakama na malipo ya deni ni baadhi ya mahitaji yanayoshindana.

Yatani alisema wakati mwingine, serikali kushindwa kufikia malengo yake ya ukusanyaji wa mapato na kusababisha kuchelewa kutoa fedha kwa baadhi ya taasisi.

"Kwa hivyo, unawezaje kuamua sasa kile kinachoenda kwa kaunti na kile kinachoenda kwingine? Utendakazi duni wa mapato yanayopatikana kitaifa huathiri malipo yetu sio tu kwa kaunti bali pia kwa idara zingine," alisema.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Waziri alitoa changamoto kwa kaunti kuacha kutegemea pesa kutoka kwa hazina ya kitaifa na kuangazia mipango ya kuzalisha mapato yake.

“Ukiangalia halmashauri za manispaa za hapo awali zilikusanya mapato mengi kuliko za sasa na hata hazikuwa na mipangilio bora na uwezo muhimu wa kusimamia fedha kama kaunti.

"Lakini sasa serikali za kaunti, zinafanya kazi kikamilifu na wataalamu wote, na miundomsingi yote na haziwezi kukusanya mapato yao wenyewe, na nadhani hilo ndilo suala tunalofaa kuhoji ni kwa nini," Yatani alisema.