Trans Nzoia: Kijana adaiwa kumuua mamake na kutupa mwili wake mtoni

Kijana huyo wa miaka 25 aliripotiwa kumuua mamake wa miaka 50 kabla ya kutorokea Eldoret.

Muhtasari

• Mwili huo ulitolewa mtoni na kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Cherangany Nursing Home katika mji wa Kitale.

Sehemu ya Mto Yala kama inavyoonyeshwa Ijumaa, Machi 25, 2022.
Sehemu ya Mto Yala kama inavyoonyeshwa Ijumaa, Machi 25, 2022.
Image: JOSIAH ODANGA

Taarifa za kusikitisha kutoka kaunti ya Trans Nzoia zinaarufu kwamba kijana mmoja alimuua mama yake na kuutupa mwili wake mtoni kabla ya kuchana mbuga kusikojulikana.

Kulingana na jarida la Nation, kijana huyo kwa jina Brian Wafula mwenye umri wa miaka 25 anadaiwa kumuua mama yake kabla ya kukisiwa kutorokea Eldoret.

“Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha Polisi cha Ushuru cha Kiminini na Bw Andrew Barasa Wanjala, 66, mume wa marehemu, Bi Judith Nafula Konya. Bi Konya, 50, alikuwa mhudumu wa maabara katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph Kitale,” Nation waliripoti.

Taarifa zinaarifu kwamba mwili wa mama huyo ulipatikana umeelea katika mto Kiminini wikendi iliyopita, siku ambayo kijana yake ambaye sasa ni mtuhumiwa alisemekana kutoweka katika kile alisema ni kutembelea mmoja wa jamaa zake mjini Eldoret.

Mumewe marehemu alisema kwamba alijaribu kumtafuta mkewe kwa simu kwa zaidi ya mara sitini bila mafanikio yoyote. Pia alijaribu kupiga simu shuleni alikokuwa anafanya kazi ila akaambiwa hayuko pale, hapo ndio ilimlazimu kuchukua hatua za kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

Mwili huo ulitolewa mtoni na kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Cherangany Nursing Home katika mji wa Kitale ambako unasubiri kufanyiwa uchunguzi. Polisi walianzisha msako dhidi ya Wafula ambaye mpaka sasa hajulikani aliko ila inaaminika yuko mjini Eldoret.