Shakahola: Miili kadhaa yakosa kubainika jinsia yao katika awamu ya pili ya upasuaji

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema kuwa miili hiyo ilikosa kubainika jinsia yao kutokana na kuharibika kupita kiasi.

Muhtasari

• Oduor alisema kuwa kati ya miili hiyo, 21 ilikuwa ya wanawake huku 10 ikiwa ni ya wanaume.

• Aidha, Oduor alisema kuwa imekuwa vigumu kubaini kiini cha vifo vya miili 22 huku kadhaa ikigundulika kuwa walifariki kutokana na kutokula chakula.

Image: BBC

Awamu wa pili ya upasuaji wa miili iliyofukuliwa katika shamba la Shakahola kaunti ya Kilifi uliendelea Jumatatu ambapo mwanapatholojia wa serikali Johansen Oduor aliongoza shughuli ya upasuaji miili 34.

Oduor alisema kuwa kati ya miili hiyo, 21 ilikuwa ya wanawake huku 10 ikiwa ni ya wanaume na mitatu iliyosalia ikikosa kubainika jinsia kutokana na kuharibika kupita kiasi.

Aidha, Oduor alisema kuwa imekuwa vigumu kubaini kiini cha vifo vya miili 22 huku kadhaa ikigundulika kuwa walifariki kutokana na kutokula chakula.

“Kwa kiini cha vifo vyao, wengi tulipata miili yao imeharibika kupita kiasi na tulishindwa kubaini chanzo cha kifo kwa maiti 22 na 12 kati yao tuliona dalili zilizoakisi kwamba huenda walifariki kutokana na njaa. Kama kawaida tulichukua sampuli kwa uchunguzi Zaidi wa DNA kwa sababu maiti nyingi zilikuwa hazitambuliki kwa hiyo sampuli hizo zitabaini jinsia yao katika maabara ya serikali,” Oduor alisema.

Mwanapatholojia huyo alibaini kwamba miili 22 ni ya watu wazima huku 12 ikiwa ya watoto.

Kufikia sasa takribani miili 50 inasubiriwa kufanyiwa upasuaji katika awamu ya pili iliyoanza wiki jana.

Ikumbukwe alipofika mbele ya kamati ya seneti inayochunguza mauaji hayo, waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki alisema kwamab wizara yake itahakikisha kwamba shughuli ya kufukua miili itaendeshwa kwa utaratibu na umakini wa hali ya juu ili kuhakikisha kwamba wanapata ushahidi wa kutosha kufanikisha kumfungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki mhubiri tata Paul Mackenzie