Nuru Okanga adai kukamatwa na DCI

“Nimekamatwa na kupelekwa Ofisi za Dci Sababu bado haijulikani,” Okanga aliandika kwenye Facebook.

Muhtasari

• “Nimekamatwa na kupelekwa Ofisi za Dci Sababu bado haijulikani,” Okanga aliandika kwenye Facebook.

• Okanga amekuwa akisifika tangu matokeo ya Cheti cha Elimu ya Msingi nchini (KCPE) kutangazwa wiki jana

ndani ya studio za Radio Jambo.
Nuru Okanga ndani ya studio za Radio Jambo.
Image: RADIO JAMBO

Mwanasiasa chipukizi Nuru Okanga ameibua dai jipya kwamba ametiwa mbaroni na makachero wa DCI na kupelekwa katika kituo kikuu cha makachero hao.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Okanga aliandika kwamba ametiwa mbaroni na yuko chini ya ulinzi katika ofisi kuu za DIC.

Hata hivyo, Okanga alisema kukamatwa kwake hakuna sababu yoyote na wala mwenyewe hajapewa sababu zozote za kukamatwa.

“Nimekamatwa na kupelekwa Ofisi za Dci Sababu bado haijulikani,” Okanga aliandika kwenye Facebook.

Okanga amekuwa akisifika tangu matokeo ya Cheti cha Elimu ya Msingi nchini (KCPE) kutangazwa wiki jana.

Mwanaharakati huyo mwenye sauti kubwa anayetazama kiti cha MCA wa Kholera, kaunti ya Kakamega alikuwa miongoni mwa watahiniwa waliofanya mitihani ya kitaifa ya shule za msingi, na Wakenya wengi walikuwa wakitazamia kujua jinsi alivyofaulu.

Okanga bado hajaeleweka kuhusu utendakazi wake katika mitihani ya KCPE, na kuwafanya baadhi ya watumiaji wa mtandao kuhitimisha kuwa huenda alijiandikisha kwa karatasi chache kuliko alivyowafanya waamini.

Mwishoni mwa wiki jana katika mahojiano kwenye stesheni ya Radio Jambo, licha ya juhudi zote za kubembelezwa, Okanga alikataa kata kata kuweka wazi alama alizozipata kwenye KCPE.

Lakini pia itakumbukwa hii si mara ya kwanza anaburuzana na mkono wa sheria.

Mtetezi huyo wa sera za ODM na Raila Odinga amekuwa akimenyana na serikali kwa kuikosoa akitumia maneno makali tena bila woga, jambo ambalo limemfanya kuwa mgeni wa makachero kila mara.