Mudavadi apongeza azma ya Ruto kudumisha amani katika mataifa mengine

Mudavadi amewahimiza wakenya kukumbatia umoja na kudumisha amani.

Muhtasari

•Musalia Mudavadi amewataka wakenya kudumisha amani huku akiwarai wakaazi wa eneo la magharibi kumuunga mkono rais Ruto kwenye ajenda zake.

•Katibu huyo pia amewataka viongozi wa eneo hilo kuchukua fursa ya uongozi wa rais Ruto na kujadiliana kupata rasilimali muhimu kwa watu wa magharibi mwa Kenya.

WAZIRI MKUU MUSALIA MIUDAVADI
Image: MUSALIA MUDAVADI/ X

Katibu mkuu wa baraza la mawaziri Musalia Mudavadi amewataka wakenya kutochukulia kawaida usalama nchini, akisema ni nguzo muhimu kwa mageuzi ya kiuchumi.

Mudavadi ambaye alikuwa akizungumza katika eneo la Kimilili, kaunti ya Bungoma mnamo Jumapili 2, alipokuwa ameungana na Rais William Ruto kwenye maombi na shukrani za madhehebu mbalimbali,alisema ni lazima wakenya wawe mstari wa mbele kuunga mkono mipango ya amani ya Rais Ruto barani Afrika.

Mudavadi alisema Rais anaongoza misheni kuu za kulinda amani na Kenya haifai wakati wowote kurejea kwenye migogoro. Alisema rais ndiye anayetetea amani na usalama katika mataifa mengine.

“Tumeona Rais akionyesha uungwana na amefikia urefu wa kumuunga mkono mshindani wake wa kisiasa katika uchaguzi uliopita Raila Odinga kwa nafasi ya uenyekiti wa umoja wa Afrika. Hii ni dalili tosha kwamba anataka kuunganisha nchi.”  Mudavadi alisema.

Aidha alitoa changamoto kwa wenyeji wa Bungoma na eneo la magharibi mwa Kenya kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Rais Ruto, akisema eneo hilo lina uwezo mkubwa ambao bado haujatumiwa. Serikali ya Ruto iko tayari kuwasaidia kutimiza malengo muhimu ya maendeleo kama kanda.

Katibu huyo pia alitoa wito kwa viongozi kutoka eneo hilo kuchukua fursa ya uongozi wa rais Ruto na kujadiliana kupata rasilimali muhimu kwa watu wa magharibi mwa Kenya.

"Lazima tuungane, kukaribiana na kuzungumza kwa sauti moja tunapotafuta suluhisho ya changamoto zinazokabili ukanda wetu." Mudavadi aliongeza. Alitaja ziara ya Rais Ruto Bungoma kama hatua muhimu ya kuimarisha uungwaji mkono kutoka eneo hilo.