Wanadada wetu wanateswa Saudi Arabia kwa ukaidi - PS Kamau Macharia

Upole na utii unaohitajika kutoka kwa wafanyikazi wa nyumbani - Macharia.

Muhtasari

• Watu wanaopata vipigo vikali, na kunyanyaswa kwa kawaida ni watu wa aina hiyo ambao ni wafanyikazi wa ndani huko - Macharia.

National Assembly//
Image: twitter

Katibu mkuu katika wizara ya mambo ya kigeni, balozi Kamau Macharia amezungumzia kitendawili cha kuteswa kwa wanadada wengi Wakenya wanaokwenda katika mataifa ya uarabuni.

Macharia alikuwa akizungumza katika hafla ya kufunzwa kwa wabunge na kutambulishwa na mambo na mifumo mbali mbali ya bungeni, hafla ambayo iko katika siku yake ya pili katika mgahawa wa Safari Park Nairobi.

Katibu huyo aliwatupia lawama wakenya hao kwa kusema kwamba baadhi yao ndio hujitakia mateso wanayolia kufanyiwa na waajiri wao. Alidokeza kwamba Wengi huwa wakaidi kwa maagizo ya waajiri wao na hivyo kujikaribishia mateso na mwisho wa siku wanaanza kulia kwamba serikali ya Kenya na ubalozi wake katika mataifa hayo upo kimya kwa suala hilo.

Macharia alisema kwa akili ya kawaida, mtu anafaa kutii amri ya mwajiri wake, kitu ambacho wengi wa wale wanaoteswa wanakaidi.

“Kuna baadhi ya maeneo upole na utii unaohitajika kutoka kwa wafanyikazi wa nyumbani sio asili kwa Wakenya wanaotafuta kazi hizo. Watu wetu huwa si watiifu na wanapokwenda katika nchi hizi kama Saudi Arabia ni zenye tamaduni za kiasili sana. Watu wanaopata vipigo vikali, na kunyanyaswa kwa kawaida ni watu wa aina hiyo ambao ni wafanyikazi wa ndani huko,” Macharia alisema.

Matamshi haya yanakuja siku kadhaa tu baada ya Wakenya kuandamana mitandaoni kulalamikia wapendwa wao kuteswa huku ubalozi ukiwa umenyamaza pasi na kutamka neno hata kidogo.