Mwanangu angekuwa muuaji angeanza na mimi - mamake Mackenzie azungumza

“Simtetei kwa sababu najua mwanangu si muuaji na hajawahi kuwa, nikisema uongo Mungu ataniadhibu,” Anastancia Mwele, mamake Mackenzie alisema.

Muhtasari

• "Hao ni wafuasi wake waliomsaliti na kuanza kusema Mackenzie ni muuaji. Alimuua nani, mbona hawatuonyeshi alimuua nani?"

• Akisimulia safari ya mtoto wake tangu utotoni, Mwele alisema Mackenzie hakumpa shida yoyote alipokuwa akikua.

Mamake Mackenzie avunja kimya kuhusu shtuma zake.
Mamake Mackenzie avunja kimya kuhusu shtuma zake.
Image: Maktaba, screengrab

Mama kwa Mchungaji mwenye utata Paul Mackenzie  kwa mara ya kwanza tangu sakala lake kuangaziwa ndani na nje ya nchi, amevunja ukimya.

Anastancia Mwele alizungumza katika runinga ya NTV na kupuuzilia mbali dhana kwamab Mackenzie ni muuaji, huku pia akisema kuwa waumini wa dhehebu lake ndio wanaomsaliti.

Anaitwa muuaji ndivyo wanavyosema, mwanangu ni muuaji, ndicho wanachokisema na bado sijawahi kuwa na tatizo naye wote wanaosema hivyo ni waumini wake unaona wanapiga mdomo,” alisema.

"Hao ni wafuasi wake waliomsaliti na kuanza kusema Mackenzie ni muuaji. Alimuua nani, mbona hawatuonyeshi alimuua nani?"

Mwele alisimulia safari ya ukuaji ya Mackenzie akiwa mtoto akisema kwamba hakuwahi mpa shida yoyote wakati anamlea na kusema kuwa aianza kama mhudumu wa teksi mjini Malindi kabla ya kufungua kanisa lake ambalo sasa limegeuka kuwa chanzo cha matatizo yake.

Mwele alisema kuwa baada ya mtoto wake kufunga kanisa lake mwaka 2019, hajawahi kusababisha matatizo yoyote.

“Simtetei kwa sababu najua mwanangu si muuaji na hajawahi kuwa, nikisema uongo Mungu ataniadhibu,” alisema.

Mamake Mackenzie alisema mwanawe hakumwambia mtu yeyote afe kwa njaa na kwamba lilikuwa chaguo la wafuasi wake kufunga.

Aliongeza kuwa habari zinazomhusu Mackenzie zilimuumiza kama mama kwa sababu zote si za kweli.

Hata hivyo, mama mtu aliitaka serikali kuendeleza uchunguzi wa haki dhidi ya mwanawe na iwapo watampata hana hatia, wamwachilie huru ili akajipambanie kimaisha.

Kakake Mackenzie alikariri maoni ya mamake, akisema hana hatia na hana uhusiano wowote na Mchungaji Ezekiel Odero wa New Life Prayer Center na Kanisa.

Kasisi Mackenzie wa kanisa la Good News International Church anachunguzwa kwa kile idara za kijasusi zinaamini kwamba mchungaji huyo alikuwa anawapa mafunzo potovu ya kidini akiwataka kujitesa njaa ya maji na chakula hadi kumuona Yesu.

Kwa sasa polisi wanafukua miili na kuwaokoa manusura katika kipande chake cha ardhi cha ekari 800 katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Hadi sasa, zaidi ya miili 100 imeopolewa kutoka kwenye makaburi ya kina kifupi msituni.