"Sina ubaya, msinikamate jamani!" Yesu wa Bungoma alia polisi wakimtaka kufika kituoni

"Mimi ninahubiri tu injili, neno la Mungu na si lingine. Hayp mengine ni uongo tu wananiwekea na ikiwa watanikamata watakuwa wamenionea."

Muhtasari

• Kuhojiwa kwake kunajiri wakati ambapo upekuzi mkali unaendelea katika kanisa la mchungaji Ezekiel.

• Jana, polisi walipata kibali cha kupiga tanji akaunti zaidi ya 15 za benki zinazohusishwa na mchungaji Ezekiel.

Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Image: Maktaba

Eliud Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren ameingiwa na tumbo joto baada ya kamanda wa polisi kaunti ya Bungoma Francis Kooli kumpa agizo la kujiwasilisha mbele yao siku ya Jumatano.

Kooli alisema kuwa wamemtaka Yesu wa Tongaren kujisalimisha kituoni mwenyewe ili kumhoji kufuatia utata ambao umekuwa ukiendelea nchini kuhusu madhehebu yanayotoa mafunzo yenye itikadi za kupotosha kwa waumini.

“Mwaliko wetu tumempa huyu ndugu tukizingatia taratibu zote za polisi. Si kwamba tumeweza kumpata na makosa yoyote lakini tunamtaka ili tuwe na mahojiano kuhusu kanisa ama dhehebu lake la kule Tongaren,” Kooli alisema.

Hata hivyo, Yesu baada ya kufikishiwa mwaliko huo alionekana kuwa na wasiwasi mwingi huku akililia asasi za kiusalama kutomkamata kwani hana hatia yoyote, akisisitiza kwamba tayari ameshafika kwa ngazi zingine za kiusalama hapo awali.

“Mimi najua kwamba hata yule kamanda wa polisi ambaye ameniita ni binadamu na ana hekima na maarifa. Naelewa kwamba anataka aniulize vile kanisa linaendelea. Huenda wanasikia mambo ambayo hayako maana kule kwa DC na kwa OCPD nimekuwa lakini sina jambo lolote,” Yesu alilia.

Pia alikanusha kwamba kuna mfuasi wa dhehebu lake ambaye ni wa kike akienda katika kanisa lake kwa maombi huwa harudi nyumbani.

“Hakuna ni uongo wananiwekea. Mimi nahubiri tu injili si linguine, ni neno tu la Mungu. Na iwapo nitakamatwa watakuwa wamenionea maana sheria hukamata wale walio na makosa, na mimi sina makosa,” alisema.