Maafisa wa zamani wa IEBC wateuliwa kwa nyadhifa za ubalozi

Muhtasari

• Consolata Nkatha, Margaret Mwachanya  na Paul Kurgat wameteuliwa kama manaibu balozi

• Hawakuwasilisha barua rasmi za kujiuzulu hadi mwezi Disemba mwaka 2018.

• Walioteuliwa kuwa mabolozi ni John Tipis, Immaculate Wambua na  Catherine Mwangi

Waliokuwa makamishna wa IEBC Margaret Mwachanya na Consolata Nkatha
Waliokuwa makamishna wa IEBC Margaret Mwachanya na Consolata Nkatha

Rais Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi aliwateua maafisa wa zamani wa tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuhudumu katika nyadhifa mbali mbali za balozi za Kenya. 

Consolata Nkatha, Margaret Mwachanya  na Paul Kurgat wameteuliwa kama manaibu balozi katika balozi za Kenya mijini Rome, Islamabad na Moscow mtawalia.

Watatu hao walijiuzulu kutoka tume ya IEBC mwezi Aprili mwaka 2018, wakitaja kutokuwa na imani na mwenyekiti Wafula Chebukati kama sababu zao za kujiuzulu. 

Hata hivyo hawakuwasilisha barua rasmi za kujiuzulu hadi mwezi Disemba mwaka 2018.

Katibu mwenza wa jopo la BBI Martin Kimani ameteuliwa kama mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika shirika la umoja wa mataifa mjini New York.

Walioteuliwa kuwa mabolozi ni John Tipis (Canberra), Immaculate Wambua (Ottawa) na  Catherine Mwangi (Pretoria). 

Jean Kamau ameteuliwa balozi mjini Addis Ababa, Linday Kiptiness (Bangkok), Tom Amolo (Berlin), Lemarron Kaanto (Brasilia), Daniel Wambura (Bujumbura) na Stella Munyi (Harare).

Wengine ni Meja Jenerali Samuel Nandwa (Juba), Meja Jenerali Ngewa Mukala (Khartoum), Benson Ogutu (Moscow), Joshua Gatimu (Tehran), Tabu Irina (Tokyo) na Jean Kimani (UN Habitat).