Wauguzi kuendelea na mgomo

Muhtasari

 • Wauguzi wameapa kuendelea na mgomo hadi pale serikali za kaunti zitakapokubali kutia saini makubaliano ya kurejea kazini.

Naibu katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Maurice Opetu
Naibu katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Maurice Opetu

Wauguzi wameapa kuendelea na mgomo hadi pale serikali za kaunti zitakapokubali kutia saini makubaliano ya kurejea kazini.

Naibu katibu mkuu wa muungano wa wauguzi nchini Maurice Opetu alisema mgomo unaondelea na ambao kufikia siku ya Jumanne ulikuwa umeingia siku ya 36 unasababishwa na ukaidi wa baraza la magavana.

“Wanachama wetu bado wako kwa mgomo katika matawi yetu yote, tunazungumza na wenzetu katika hospitali ya MTRH na ile ya kitaifa ya Kenyatta kuungana nasi,” Opetu alisema.

Aliongeza kuwa masaibu ambayo wakenya wanapata katika sekta ya afya sio makossa ya wahudumu wa afya bali ni kwa sababu baraza la magavana limekataa kutia saini makubaliano ya kurejea kazini.

Alikanusha madai ya baraza la magavana kuwa hawakuhusika katika majadiliano ya kupata mwafaka wa kurejea kazini yaliyoongozwa na waziri wa afya Mutahi Kagwe.

Kulingana na Opetu baraza la magavana liliwakilishwa katika mkutano wa pamoja uliyopata mwafaka wa kurejea kazini.

Alimpongeza waziri wa afya Mutahi Kagwe kwa juhudi zake kuleta mwafaka ili kumaliza mgomo wa wahudumu wa afya ingawa anashtumu serikali za kaunti kwa kuhujumu juhudi hizo.

Muungano wa  wauguzi unasema kwamba uko tayari kufanya mgomo hata kwa mwaka mzima ikiwa matakwa yao hayatashughulikiwa.

“Hatutarudi kazini, tunataka rais kuingilia kati swala hili   ili kukwamua utata uliyoko wauguzi wanafaa kukaa ngumu hadi mwafaka upatikane” Opetu alisema.

Alifichua kwamba baadhi ya wauuguzi hawajapokea mishara yao kwa miezi 16 sasa.