Wanahabari wataka kuzingatiwa katika awamu ya kwanza chanjo ya Covid-19

Muhtasari

• KUJ yamuandikia barua waziri wa afya Mutahi Kagwe kutaka wanahabari kwa hiari yao kupewa chanjo ya covid-19.

• Takriban watu milioni 1.25 wanatarajiwa kupokea chanjo hiyo nchini Kenya katika awamu ya kwanza.

Chama cha kutetea haki za wanahabari nchini Kenya (KUJ) kinataka wanahabari pia kujumuishwa katika makundi ya kwanza kupokea chanjo ya covid-19.

Katibu mkuu wa KUJ Eric Oduor siku ya Jumatano alisema kwamba wanahabari pia wanakabiliwa na hatari kubwa kuambukizwa virusi vya corona wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Chama hicho tayari kimemuandikia barua waziri wa afya Mutahi Kagwe kikitaka wanahabari kwa hiari yao kupewa chanjo ya covid-19 katika awamu ya kwanza ya kutolewa kwa chanjo hiyo.

 

“Hatuwezi tu kuitwa wafanyikazi wa mstari wa mbele wakati huduma zetu zinahitajika kueneza habari muhimu na kuhamasisha umma kuhusu covid-19, lakini ukifika wakati wa kupokea chanjo wanahabari tunaachwa nje,” Eric Oduor alisema.

Shehena ya kwanza ya takriban chanjo milioni moja za AstraZeneca ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa JKIA usiku wa kuamkia Jumatano na kupokelewa na waziri wa Afya Mutahi Kagwe miongoni mwa viongozi wengine wakuu katika serikali.

Chanjo hiyo ya AstraZeneca iliagizwa kutoka taasisi ya Serum ya India.

Serikali ilitangaza kwamba wahudumu wa afya watakuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo ili kupata kinga ya kutosha dhidi ya virusi hivyo wanapo wahudumia wakenya.

Watu wengine katika makundi ya kwanza kupokea chanjo hiyo kulingana na ratiba ya wizara ya afya ni walimu, maafisa wa usalama wahudumu wa mahoteli, watu wenye afya duni na maafisa wa uhamiaji.

Akipokea chanjo hiyo katika uwanja wa JKIA, Waziri wa afya Mutahi Kagwe alisema kwamba..."Kwa kweli ni siku njema kwa Kenya. Sasa tuna silaha sawia na bazooka au machine gun katika vita vyetu dhidi ya virus.

Takriban watu milioni 1.25 wanatarajiwa kupokea chanjo hiyo nchini Kenya katika awamu ya kwanza.