Mhubiri akubaliwa na mahakama kutwaa mtoto aliyetelekezwa kwenye reli

Mahakama ya Milimani mjini Nairobi
Mahakama ya Milimani mjini Nairobi

Mahakama ya mjini Nairobi imemruhusu mchungaji mwenye umri wa makamo kutwaa mtoto aliyeachwa miaka minne iliyopita kwenye reli katika vitongoji duni vya Dandora.

Mchungaji huyo aliyefiwa na mumewe miaka 9 iliyopita ni mama wa mtoto wa miaka 32 ambaye pia amekubali mama yake kumchukua mtoto huyo.

Jaji Maureen Odero alisema kuwa mchungaji huyo anayeendesha kanisa moja jijini Nairobi ameihakikishia korti kwamba mtoto wake wa kiume na jamaa wa karibu wanaunga mkono wazo la kumchukua mtoto huyo.

Jaji Odero pia alisema mtoto wa Mchungaji alikuwa amejulisha korti kwamba alikuwa akifahamu fika kwamba baada ya kupitishwa kwa mtoto ambaye sasa ni kaka yake, atakuwa na haki zote sawia na za mtoto aliyezaliwa na mchungaji huyo ikiwa ni pamoja na haki ya urithi.

Mahakama iliamua kwamba kwa kuwa juhudi za kutafuta jamaa za mtoto huyo zilikuwa zimeambulia patupu mama huyo huyo alikuwa radhi kumchukuwa mtoto huyo kwa makao ya watoto.  

"Badala ya mtoto kuishi maisha ya kutokuwa na uhakika kuhusu wazazi wake akiwa katika makao ya watoto ni vyema achukuliwe na mzazi mwingine" korti iliamua.

Jaji Odero alisema kupitishwa kutampa mtoto huyo nafasi ya kulelewa katika nyumba ya upendo wa Kikristo.

Jaji aliongeza kuwa amehoji mtoto huyo mtandaoni na aliweza kutaja jina lake na shule ya chekechea.

"Ushahidi wa mshikamano kati ya mtoto na familia ulikuwa wazi kwangu kwani alikuwa amekaa vizuri kwenye mapaja ya mtoto mzima wa mwombaji, alikuwa mchangamfu na alionekana kutunzwa vizuri" korti ilisema.

Kulingana na rekodi za mahakama, mtoto huyo anaaminika kutelekezwa mwezi Agosti 2016 muda mfupi baada ya kuzaliwa huko Dandora.

Aliokolewa na msamaria mwema na baadaye akapelekwa nyumbani kwa watoto.

Mtoto huyo kisha aliwekwa katika malezi ya wazazi na ndivyo alikutana na mchungaji ambaye alimchukua kama mlezi na mwaka jana aliomba kumchukuwa.

"Kutokana na ushahidi uliotolewa kortini nimeridhika kuwa mwombaji ni mzazi anayefaa kulea" Jaji Odero alisema.