COVID-19: Zaidi ya walimu 40 wamefariki, TSC yazindua chanjo

Muhtasari

• Kulingana na takwimu za TSC zaidi ya walimu 40 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya COVID-19.

• Walimu watakaosimamia mitihani ya kitaifa – KCPE na KCSE pia watapewa kipau mbele katika chanjo hizo.

Afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia ajiandaa kupokea chanjo ya COVID-19
Afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia ajiandaa kupokea chanjo ya COVID-19
Image: DOUGLAS OKIDDY

Takriban walimu 15,000 wenye umri wa zaidi miaka 50 wanatarajiwa kupokea chanjo ya COVID-19 kuanzia wiki ijayo.

Tume ya kuajiri walimu nchini TSC siku ya Alhamisi ilizindua zoezi hilo ambalo linalenga kuwapa walimu kinga ya kutosha wanaposhughulikia wanafunzi .

Afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia alisema zoezi hilo litajumuisha walimu wote wakiwemo wale katika shule za kibinafsi. Alikariri msimamo wa serikali kutobagua walimu katika shule za kibinafsi.

Alisema walimu watakaopokea chanjo katika awamu ya kwanza ni wenye umri wa miaka 50 kwenda juu na wale walio na matatizo ya kiafya.

 

Kulingana na takwimu za TSC zaidi ya walimu 40 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya COVID-19.

Walimu watakaosimamia mitihani ya kitaifa – KCPE na KCSE pia watapewa kipau mbele katika chanjo hizo ingawa TSC imebaini kuwa chanjo hiyo itatolewa kwa hiari.

Mwaka huu, Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) linasema jumla ya wasimamizi na wasahihishaji 286,901 watapewa kandarasi ya usimamizi wa mitihani ya KCPE na KCSE.

Wasimamizi na wasahihishaji huchaguliwa kutoka kwa walimu waliosajiliwa na tume ya TSC.

Ikiwa pendekezo la kujumuisha maafisa wa mitihani katika chanjo hiyo litakubaliwa, itamaanisha kuwa idadi kubwa ya walimu nchini watakuwa wamepewa chanjo katika awamu hii ya kwanza.

Hivi sasa, nchi ina idadi ya waalimu 387,000 katika shule za umma na wengine 150,000 katika shule za kibinafsi.

Chanjo hiyo itafanyika katika vituo vya mitihani.