Kaunti ya Kisumu yaweka mikakati mikali kudhibiti maambukizi ya COVID 19

Mili ambayo haitakuwa imechukuliwa kwenye vyumba vya kuhifadhi maiti baada ya masaa 48 kuisha itazikwa katika makaburi ya umma bila kuarifu familia

Muhtasari

•Ofisi za kaunti hiyo zitabaki zimefungwa kwa muda usiojulikana isipokuwa kwa huduma muhimu. 

•Kaunti ya Kisumu imeripoti visa 5739 vya COVID 19 kufikia sasa huku visa vingi vikiripotiwa kwa kipindi cha wiki nne zilizopita.

Gavana wa Kisumu Anyang Nyong'o
Gavana wa Kisumu Anyang Nyong'o

Kaunti ya Kisumu imeweka mikakati mikali ya kukabili kuenea kwa virusi vya Korona kufuatia ongezeko kubwa ya visa vya COVID 19 kuripotiwa.

Mkutano uliofanyika siku ya Jumatatu ukiongozwa na gavana Anyan'g Nyong'o na msaidizi wa kamishna wa kaunti wa Kisumu ya Kati, John Cheruiyot ulizungumzia namna ya kukabili virusi hivyo na kutangaza mikakati mpya itakayofuatwa katika kaunti hiyo.

Mkutano huo uligusia sana swala la kuhifadhiwa kwa mili ya wafu na namna ya kufanya mazishi.

Vyumba vya kuhifadhia maiti vimeagizwa kutoweka mili kwa zaidi ya masaa 48 huku mili ambayo haitakuwa imechukuliwa kabla ya masaa hayo kuisha ikitangazwa izikwe katika makaburi ya umma bila kuarifu familia.

Vyumba hivyo pia vimeagizwa kutochukua mili kutoka nje ya hospitali ila tu inayohusiana na visa vya polisi. Wafu wote wametangazwa kuzikwa kabla ya masaa 72 kuisha huku mazishi yakihudhuriwa na watu wasiopita 100.

Ofisi za kaunti hiyo zitabaki zimefungwa kwa muda usiojulikana isipokuwa kwa huduma muhimu. Wakazi wa kaunti hiyo pia wameshauriwa kutohudhuria ibada kwenye vyumba vya kuabudu.

Kaunti ya Kisumu imeripoti visa 5739 vya COVID 19 kufikia sasa huku visa vingi vikiripotiwa kwa kipindi cha wiki nne zilizopita.

Asilimia ya maambukizi katika kaunti hiyo kwa sasa ni 28.4%.Inasemekana kuwa maambukizi ya sasa yako na madhara zaidi yakilinganishwa na mwaka uliopita. Asilimia 78% ya visa vinavyoripotiwa vinasemekana kuwa na madhara kali.

Kaunti hiyo inarekodi takriban vifo 12 kila wiki.