Oguna atetea makaribisho baridi ya kikosi cha Olimpiki

Muhtasari

• Akiongea mtaani Mukuru kwa Reuben siku ya Alhamisi, Oguna alisema serikali inajivunia wanariadha wake licha ya mapokezi baridi.

• Wakenya walitumia mitandao ya kijamii kuelezea kusikitishwa kwao na mapokezi ambayo wanariadha walipokea nchini waliporudi kutoka Japani Jumatano.

Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna amesema wanariadha wa Kenya walioshiriki kwenye michezo ya Olimpiki mjini Tokyo Japan hawakupewa mapokezi ya hadhi kwa sababu ya itifaki za Covid -19.

Akiongea mtaani Mukuru kwa Reuben siku ya Alhamisi, Oguna alisema serikali inajivunia wanariadha wake licha ya mapokezi baridi.

"Ilikuwa wakati wa kujivunia na watu huwa wanakosa umakini. Itifaki za Covid-19 lazima zingezingatiwa hata kwenye uwanja wa ndege, ”alisema.

Oguna alisema kikosi cha Tokyo kilikuwa kimepeperusha bendera ya Kenya juu na serikali inajivunia wanariadha.

“Kenya ilikuwa katika nafasi ya 19 katika mashindano hayo ulimwenguni na ilikuwa ikiongoza barani Afrika. Tunajivunia kama Serikali ya Kenya kwa juhudi nzuri wanariadha walizoweka Tokyo, ”akaongeza.

Wakenya walitumia mitandao ya kijamii kuelezea kusikitishwa kwao na mapokezi ambayo wanariadha walipokea nchini waliporudi kutoka Japani Jumatano.

Nchini Uganda, Rais Yoweri Museveni alikabidhi magari ya hadhi kwa kila mmoja wa washindi wa medali katika Olimpiki, akiongeza kuwa serikali itawajengea nyumba wazazi wa washindi wa dhahabu.