Kijana ahukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kuvunja televisheni za mama yake Lang'ata

Muhtasari

•Ronald Kipkemoi alikubali mashtaka ya kuharibu televisheni aina ya Haier ya inchi 55  na nyingine aina ya Sony Bravia ya inchi 28 zenye thamani ya shilingi 95,000.

•Mshukiwa aliambia hakimu  William Tulel kwamba aliamua kufanya uharibifu huo kwa kuwa mama yake hampendi.

court
court

Habari na Clause Masika

Kijana mmoja kutoka mtaa wa Lang'ata kaunti ya Nairobi atalazimika kula kalenda kwa kipindi cha miezi sita baada ya kukiri kuharibu televeshini mbili zilizomilikiwa na mama yake.

Alipofikishwa mbele ya mahakama ya Kibera, Ronald Kipkemoi alikubali mashtaka ya kuharibu televisheni aina ya Haier ya inchi 55  na nyingine aina ya Sony Bravia ya inchi 28 zenye thamani ya shilingi 95,000.

Kipkemoi anadaiwa kutekeleza uhalifu huo akiwa nyumbani kwao katika mtaa wa Lang'ata mnamo Oktoba 25.

Aliambia hakimu  William Tulel kwamba alifanya uharibifu huo kwa kuwa mama yake, Ruth Chelimo hampendi.

Mzozo uliibuka baada ya Kipkemboi kutumia bodaboda kuenda nyumbani, huduma ambazo alitaka mama yake alipie.

Kwa kuwa mama yake hakuwa na pesa mkononi aliamua kulipa kutumia Mpesa, jambo ambalo halikumpendeza Kipkemboi.

Kipkemboi  alianza kumgombeza mama yake huku  akidai kwamba mama yake alikataa kulipa kwa kuwa hampendi.

Kutokana na hasira aliyokuwa nayo aitishia kuvunja televisheni iliyokuwa sebuleni na iliyokuwa kwenye chumba cha mama yake cha kulala na akaendelea kutekeleza vitisho vyake.

Kufuatia hayo Bi. Chelimo aliamua kuripoti mwanawe katika kituo cha polisi cha Langata na hapo Kipkemboi akakamatwa.

Televisheni ambazo mshukiwa aliharibu zilitumika kama ushahidi mahakamani.

Kipkemboi alikubali mashtaka dhidi yake na akahukumiwa kifungo bila chaguo la dhamana.