Jaji aliyemhukumu DCI Kinoti ahofia maisha yake

Muhtasari

• Nilishangaa kufikiwa na mjumbe aliyetumwa na afisa mmoja wa serikali,” Mrima alisema. 

• Jaji hakutaja suala ambalo alishughulikia hasa lakini alisema mjumbe huyo alikuwa na ujumbe mmoja wazi: kwamba anapaswa kuacha ubinafsi na kuacha kutoa kile kilichoelezwa kuwa 'amri zisizofaa'. 

Jaji wa Mahakama Kuu Antony Mrima. Picha: MAHAKAMA YA KENYA
Jaji wa Mahakama Kuu Antony Mrima. Picha: MAHAKAMA YA KENYA

Jaji wa Mahakama Kuu, Anthony Mrima amedai kwamba amekuwa akitishiwa na maofisa wakuu wa serikali kwa kile kilichotajwa kuwa anatoa “amri zisizopendeza” dhidi ya Serikali. 

Mrima alisema hayo alipokuwa akitoa uamuzi siku ya Alhamisi ambapo alimhukumu Mkurugenzi wa DCI George Kinoti kifungo cha miezi minne gerezani, kwa kukosa kutii amri ya mahakama iliyomtaka kurejesha bunduki za mfanyabiashara Jimi Wanjigi. 

“Hivi majuzi nilishughulikia jambo na kutoa maagizo. Maagizo hayo yalielekezwa kwa baadhi ya maafisa wakuu wa serikali. Nilishangaa kufikiwa na mjumbe aliyetumwa na afisa mmoja wa serikali,” Mrima alisema. 

Jaji hakutaja suala ambalo alishughulikia hasa lakini alisema mjumbe huyo alikuwa na ujumbe mmoja wazi: kwamba anapaswa kuacha ubinafsi na kuacha kutoa kile kilichoelezwa kuwa 'amri zisizofaa'. 

Mrima anasema ujumbe huo haukuishia hapo kwani alifahamishwa zaidi kuwa asipozingatia onyo hilo, atachukuliwa hatua kali kwa kutumia michakato mingine mingi waliyonayo. 

"Mimi si mgeni kwa vitisho hivyo na vitendo halisi vya ukatili dhidi yangu," alisema. 

Mrima aliongeza kuwa wakati wa uchaguzi uliopita, alishughulikia maombi ya kura ambapo wajumbe kadhaa walitumwa kwake wakiwa na maelekezo ya namna ya kuamua ombi la uchaguzi.