Mwanaharakati wa LGBTQ Chiloba kuzikwa Jumanne-Familia imesema

Washukiwa watano wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.

Muhtasari
  • Chiloba alipatikana ameuawa na mwili wake kuhifadhiwa kwenye sanduku la chuma ambalo lilitupwa katika kijiji cha Hurlingham karibu na Kipkaren nje kidogo ya Mji wa Eldoret
Mwanaharakati wa LGBTQ, Chiloba
Mwanaharakati wa LGBTQ, Chiloba
Image: Instagram

Mwili wa mwanaharakati wa LQBTQ aliyeuawa Edwin Kiprotich kiptoo almaarufu Chiloba utaondolewa kesho(Jumanne) katika chumba cha kuhifadhi maiti cha MTRH na kupelekwa moja kwa moja nyumbani kwa mazishi.

Familia yake inasema watazikwa katika kijiji cha Sergoit kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Binamu yake Gladys Chiri alisema mipango ya maziko ilikuwa imekamilika na familia itakuwa katika chumba cha maiti kufikia saa nane asubuhi ili kuuchukua mwili huo.

"Tutaelekea nyumbani moja kwa moja kwa ibada ya familia kisha mazishi," alisema.

Hata hivyo familia haijatoa maelezo ya kina kuhusu mazishi hayo na ni nani atahudhuria.

Chiloba alipatikana ameuawa na mwili wake kuhifadhiwa kwenye sanduku la chuma ambalo lilitupwa katika kijiji cha Hurlingham karibu na Kipkaren nje kidogo ya Mji wa Eldoret.

Washukiwa watano wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.

Miongoni mwao ni mshukiwa mkuu Jacktone Odhiambo ambaye aliishi na Chiloba eneo la Kimumu kando ya barabara ya Eldoret Iten.

Washukiwa hao watafikishwa mahakamani Januari 31 pengine kufunguliwa mashtaka baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kimahakama wa mauaji hayo.

Jozi tatu za soksi na vipande vingine vya nguo vilitolewa mdomoni mwa marehemu wakati wa zoezi la uchunguzi wa maiti iliyotekelezwa na mtaalamu mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor.

Dkt Oduor alieleza kuwa Chiloba alifariki kwa kuzibwa mdomo hali iliyomfanya kukosa oksijeni.

Katika visa vingi ndani ya miili ya jamii ya Wakalenjin hupelekwa nyumbani siku moja kabla ya mazishi lakini Chiloba atazikwa siku hiyo hiyo.