Herman Manyora aonya dhidi ya Raila kupoteza kura kwenye ngome yake huko Nyanza

Muhtasari

• Manyora amesema Raila anapaswa kuwa makini kuhusu wagombea anaowapa tikiti ya ODM maeneo hayo.

• Amemtaka kutoa nafasi kwa wakazi kuchagua viongozi wao wanaowataka.

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa, Herman Manyora amemuonya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga kuhusu uwezekano wa kupoteza kura huko Nyanza iwapo hatabadilisha mbinu zake za kisiasa.

Manyora amemtaka Odinga kufanya mashauriano na wakazi wa maeneo hayo ili kufahamu kiongozi wanayemtaka wala sio yule wa kulazimishiwa kwao.

Alisema kwamba hatua ya kutoa tikiti ya moja kwa moja kwa baadhi ya wagombea, itapelekea chama hicho cha ODM kukataliwa na kupoteza kura muhimu.

"...Ni sawa pengine anataka kumchagua mtu ambaye ni mwaminifu kwake, ila lazima awe makini na kuzingatia hisia za wakazi pia." Manyora alisema.

Huku ikiwa wazi kwamba kuna wagombea kadhaa ambao watakuwa wanaingia katika kura za mchujo kupitia chama cha ODM, Manyora alimtaka Raila kufanya mashauriano ya kina na wagombeaji hao ili kuhakikisha kunakuwa na umoja mbele ya uchaguzi wa Agosti 9, na kuhakikisha wanampta mtu faafu atakayewakilisha kambi hiyo.

Aidha, alimtaka Raila kukoma kuwalazimisha wandani wake kugombea nyadhfa mbalimbali kwa kile alichokitaja kwamba huenda hatua hiyo ikachangia yeye kupoteza kura za urais.

"...Unajua hata hao watu watajiuliza mbona huyu jamaa anatulazimishia watu, kwa hiyo lazima apige hesabu sana," aliongezea.

Huku kura za mchujo zikitarajiwa kung'oa nanga mwezi huu wa Aprili, inasubiriwa kuona chama hicho kitatumia mbinu gani katika mchakato wa kutoa tikiti kwa wagombea wake.