(VIDEO) Wafanyakazi wa Ruto waandamana kulalamikia kucheleweshwa kwa mishahara

Muhtasari

• Wafanyakazi katika shamba linalohusishwa nac naibu rais William Ruto waliandamana Jumatatu kulalamikia kucheleweshwa kwa marupurupu yao ya kati ya shilingi 300 hadi 500 kwa siku.

Waandamanaji nje ya lango la shamba la Kisima, Taita Taveta
Waandamanaji nje ya lango la shamba la Kisima, Taita Taveta
Image: Screengrabs: Nation

Shughuli katika shamba moja huko Mata kaunti ya Taita Taveta linalohusishwa na naibu wa rais William Ruto zilitatizika Jumatatu baada ya wafanyakazi kugoma na kufanya maandamano ya amani wakilalamikia kucheleweshwa kwa marupurupu yao.

Wafanyakazi hao waliandamana nje ya lango kuu la kuingia shambani humo kwa kile waliteta vikali kwamba ni ahadi zisizotimizwa kuhusu mishahara na marupurupu yao na uongozi wa shamba hilo linalohusishwa na naibu wa rais.

Wafanyakazi hao ambao marupurupu yao yanaanzia kati ya shilingi 300 hadi 500 pesa za Kenya kwa siku, walisema mishahara yao imecheleweshwa kwa miezi kadhaa pasi na kupewa sababu maalumu kuhusu kucheleweshwa kwenyewe.

Mgomo huu wa wafanyakazi wa shamba linalohusishwa na naibu rais William Ruto unakuja kipindi ambapo Ruto anaendeleza misururu ya kampeni zake za kumrithi rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi katika uchaguzi wa Agosti 9, huku akimwaga mamilioni ya pesa katika hafla mbalimbali za michango na maeneo ya ibada, wakati wafanyakazi wake wanalilia kucheleweshwa kwa shilingi 300 zao za kila siku.

Ni kinaya kwamba wafanyakazi wa chini katika shamba hilo la Kisima linalohusishwa na mgombea urais huyo wanalalama kuhusu marupurupu hali ya kuwa mwajiri wao mkuu anaeneza kampeni kila kona ya nchi kwamba moja ya ajenda zake kuu ni kuinua na kuboresha maisha ya watu wa chini kama hao, akiwaita kwa jina la jumla kama ‘hustlers’