"Umeniangusha sana!" Karen Nyamu amuambia MC Jessy kwa kubadili msimamo

Muhtasari

• Karen Nyamu amedhihirisha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa MC Jessy kuwania ubunge kama mgombea huru baada ya kuondoka UDA.

Karen Nyamu
Karen Nyamu
Image: Facebook

Aliyekuwa anawania kiti cha useneta Nairobi, Karen Nyamu ameonesha wazi kukwazika kwake na uamuzi wa mchekeshaji Jasper Muthomi kuamua kuwania ubunge wa Imenti ya Kusini kama mgombea huru.

Nyamu aliandika kupitia Facebook yake na kuonesha kuvunjika moyo kwa uamuzi huo ambapo amesema mchekeshaji huyo anayetambulika na wengi kama MC Jessy amekubali kudanganywa na kuacha kazi aliyokabidhiwa katika kampeni za naibu rais baada ya kushawishiwa kuacha kuwania tiketi ya UDA na kukabidhiwa Mwiti Kathaara.

“MC Jessy rafiki yangu mkubwa, sasa mbona umekubali mbogi ya mtupe nimsanye wakuingize? Afathali ungekaa ngumu pale kwa meza ya mazungumzo badala ya kugonga dili kisha kughairi, haidhuru, Kama kawaida ninakutakia kila la kheri na kuheshimu azimio lako la hivi punde,” alilalama Karen Nyamu kupitia Facebook yake.

Nyamu pia alikuwa analenga kuwania tiketi ya UDA kuwania useneta wa Nairobi lakini baada ya mazungumzo ya kina na kinara wa chama, William Ruto, alishawishiwa na kukubali kuachia nafasi hiyo mwanamama Askofu Margaret Wanjiru ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mbunge wa Starehe jijini Nairobi.