Karua awaonya wanasiasa dhidi ya vurugu, matusi wakati wa kampeni

Muhtasari
  • Karua awaonya wanasiasa dhidi ya vurugu, matusi wakati wa kampeni
Martha Karua
Image: MARTHA KARUA/TWITTER

Mgombea mwenza wa urais wamuungano wa Azimio La Umoja  Martha Karua amewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kutumia vurugu na matusi wanapoendesha kampeni zao.

Karua, alipokuwa akizungumza katika ziara ya kampeni mjini Nakuru siku ya Jumamosi, alikosoa viongozi kwa kutumia lugha chafu na kuwarushia matusi walio mamlakani ili kupata mafanikio makubwa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

Kiongozi huyo wa chama cha NARC Kenya alidokeza kuwa kutomheshimu rais au gavana aliyeketi huku akitafuta wadhifa sawa kunaweza kutokea tena kwa viongozi wale wale watakapopanda nyadhifa hizo.

“Mambo ya fujo na matusi tumekataa; ukitaka urais, lazima uheshimu rais aliyopo. Mkosoe, lakini kwa njia ya heshima ndivyo wewe ukiingia tuweze kukuheshimu,” Karua alisema.

“Ukitaka ugavana heshimu gavana alioko, hatusemi usimkosoe, mkosoe lakini kwa njia ya heshima.”

Huku akiendelea kuwashawishi wapiga kura kuunga mkono mgombeaji kinara wa Azimio Raila Odinga, Karua alitoa wito kwa wakazi kuwaepuka wanasiasa wanaopeana zawadi na kuzingatia wale walio na rekodi ya uadilifu na ubora.

Alionyesha ubaya wa takrima akitaja enzi ya marehemu Rais Mwai Kibaki akisema kwamba wakati wa muhula wake, ingawa hakuwa ametoa takrima ili kupigiwa kura, uchumi ulistawi baada ya kushika madaraka.

“Wacha kutishwa na pesa ya mtu…ata akiwa ni tajiri wa mwisho, haiwezi kutosha Wakenya. Sijawahi skia tajiri akisema watoto wa kijiji chake waende shule ata kwa term moja pekee, ama akisema hospitalini watu wakunywe dawa wiki mpja. Sijaskia pesa ikitosha wananchi lakini kodi yetu sisi sote inaweza kututosha,” Karua alisema.