Junet aishtumu kambi ya Ruto kwa kujaribu kushawishi kikao cha bunge

Junet alidai kuwa timu ya Ruto ilipanga njama ya kutumia uhusiano wao na Spika Muturi kuteua karani.

Muhtasari

•Junet alidai kuwa timu ya Ruto ilipanga njama ya kutumia uhusiano wao na Spika Justin Muturi kuteua karani haraka kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

•Muturi alipuuzilia mbali madai ya timu ya Azimio akisema kuwa wabunge bado wako kazini licha ya kuwa katika mapumziko kwa kampeni.

JUNET.
JUNET.
Image: HISANI

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed mnamo Jumatatu, Julai 11 alidai kuwa wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza walikuwa na mpango wa kuteua karani wakati wa kikao maalum  cha bunge kitakayofanyika Julai 13.

Akihutubia wanahabari, Kiranja huyo wa wachache bungeni alidai kuwa timu ya Naibu Rais William Ruto ilipanga njama ya kutumia uhusiano wao na Spika Justin Muturi kuteua karani haraka kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

Alidai kuwa timu ya Kenya Kwanza ilipanga kupenyeza ajenda ya Karani katika majadiliano ya bunge baada ya mjadala kuhusu Muswada wa Huduma.

Junet alieleza kuwa mpango wa timu ya Kenya Kwanza ulikuwa sehemu ya mkakati wao wa kutatiza ajenda ya serikali katika Bunge iwapo Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga atashinda uchaguzi wa Agosti 9.

Zaidi ya hayo,  mbunge huyo  alitaka kujua kwa nini Muturi hakuandika kwenye gazeti la serikali notisi kuhusu kikao hicho maalum kulingana na sheria.

''Kuna umuhimu gani wa kuitisha Bunge kwa kikao maalum cha kuteua Karani mpya kwa siku chache tu kabla ya uchaguzi na bila taarifa ya Gazeti? Haiwezi kufanywa badaye '' Mbunge huyo alihoji.

Hata hivyo, Muturi alipuuzilia mbali madai ya timu ya Azimio akisema kuwa wabunge bado wako kazini licha ya kipindi cha mapumziko kwa kampeni kung'oa nanga.

"Siku zote nimekuwa nikichukia siasa za Wabunge ambao hawana hakika kwa yale wanasema, na si haki kwa mtu yeyote kutoa madai kama hayo." Muturi alisema.

Alieleza kuwa aliitisha kikao hicho kwa mujibu wa taratibu za Bunge na kuongeza kuwa walikuwa na shughuli zinazosubiri kutekelezwa.

Muturi aliongeza kuwa bado hajaegemea upande wowote katika kutekeleza majukumu yake bungeni licha ya kuwa kwa timu ya Ruto.

Alisema madai hayo hayana msingi na yalitengenezwa na timu ya Azimio ili kumchafua kwa sababu ya mwelekeo wake wa kisiasa.

“Niko uwanjani kumpigia debe mgombeaji urais ninayempenda William Ruto'' alisema.

Wabunge wanatarajiwa kumchagua karani mpya kufuatia kuteuliwa kwa karani wa sasa- Michael Sialai kama Kamishna Mkuu wa Kenya nchini Namibia.