Sijiskii salama tena! Bahati ahofia maisha yake baada ya kukataa ofa ya kazi ya Raila

Bahati alidai kuwa mpinzani wake alituma wahuni kumshambulia baada ya kufanikiwa kuingia mkutano wa Azimio.

Muhtasari

•Bahati almemshtumu mpinzani wake kwa kutuma wahuni waliomshambulia na kurarua nguo zake. 

•Pia aliweka wazi kuwa hataki kazi ambayo aliahidiwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga ikiwa atatwa urais.

Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Msanii Bahati Kelvin Bahati Kioko anayelenga ubunge Mathare kupitia chama cha Jubilee
Image: Instagram screenshot

Mgombea ubunge wa Mathare kwa tiketi ya Jubilee Kelvin 'Bahati Kioko sasa anadai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Jumatatu asubuhi mwimbaji huyo alipakia video iliyorekodiwa nyumbani kwake akisimulia masaibu aliyokumbana nayo Jumapili.

"Nilidhani nahitaji kusema haya.. Sihisi salama tena. Lakini nitapigana kwa ajili ya watu wa Mathare hadi mwisho," Bahati aliandika chini ya video hiyo ambayo alidai ilirekodiwa saa saba usikuwa kuamkia Jumatatu.

Katika video hiyo 'mtoto wa mama'  alimshtumu mpinzani wake kwa kutuma wahuni waliomshambulia na kurarua nguo zake. 

Alidai kuwa mpinzani wake ndiye aliyesababisha matatizo mengi kwenye azma yake ya kuwania ubunge wa Mathare.

"Alitaka ninyang'anywe tiketi nikapewa, upande mwingine akaleta propaganda eti nimejiondoa na nikakataa, akataka nipatiwe kazi nayo pia nimekataa. Leo kwa lazima niwe jasiri na nifanye ninachohitajika kufanya kwa sababu napigania watu wa Mathare.. " Alisema katika video hiyo ya dakika mbili unusu.

Bahati alidai kuwa mpinzani wake alituma wahuni kumshambulia baada ya kufanikiwa kuingia kwenye mkutano wa Azimio-One Kenya.

"Amekuwa akinitishia. Leo ametuma wahuni. Wameniacha hivi... Hivi ndivyo wamefanya shati yangu ya Jubilee. Alituma watu wanishambulie na kujaribu kunisimamisha... Hivi ndivyo ameamua kufanya siasa zake," Mwanamuziki huyo alisema huku akionyesha shati yake iliyoraruka. 

Pia aliweka wazi kuwa hataki kazi ambayo aliahidiwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga ikiwa atatwa urais.

Alibainisha kuwa tayari ana kazi ya muziki na kudai alijitosa kwenye siasa baada ya kuona wanazopitia wakazi wa Mathare.

"Niko na kazi kama mwanamuziki lakini watu wangu wa Mathare bado wanaishi maisha ambayo siwezi kueleza," Alisema.

Jumapili Raila alipokuwa anajipigia debe katika eneo la Mathare alimuidhinisha Oluoch kuwania ubunge wa eneo hilo na kuahidi kumpa Bahati kazi katika serikali yake ikiwa atachaguliwa kuwa rais mnamo Agosti 9.

"Huyu Bahati ni mtoto yangu. Yeye nitampatia kazi katika serikali. Sawasawa. Kwa hivyo sasa mbunge wa Ruaraka ni bwana TJ Kajwang, halafu mbunge wa Mathare ni bwana Oluoch," Raila alisema.

Baadae hata hivyo Bahati alizama kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kusisitiza kuwa hatatupilia azma yake ya kuwania ubunge.

"Nimeidhinishwa na IEBC na chama changu cha Jubilee.. Nimebarikiwa na Mungu na watu wa Mathare wameamua mbunge anayefuata ni Bahati Kioko," Bahati aliandika kwenye Twitter.

Aliendelea "Mimi Bahati Kioko nitakuwa kwenye debe mnamo Agosit 9!"

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 29 anatazamia kumbandua Oluoch ambaye ndiye  anayekalia kiti cha ubunge wa Mathare.