Kwani vita vya Ukraine vimekwisha? Ruto amsuta Uhuru kwa kushusha bei ya unga

Ruto alidai kuwa Serikali imepunguza bei hizo kama hatua ya kuwahadaa wapiga kura

Muhtasari

•Ruto, bila kutaja majina, alimkemea Uhuru kwa kulaumu vita vya Ukraine na Urusi kwa gharama ya juu ya maisha.

•Ruto alidai kuwa Serikali imepunguza bei hizo kama hatua ya kuwahadaa wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 

alipokuwa kwenye kampeni katika Kaunti ya Nairobi mnamo Julai 18,2022.
Kiongozi wa UDA William Ruto alipokuwa kwenye kampeni katika Kaunti ya Nairobi mnamo Julai 18,2022.
Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Mgombea urais wa UDA William Ruto amemkejeli Rais Uhuru Kenyatta kwa kufidia bei ya unga wa mahindi.

Akizungumza Jumatatu wakati wa kampeni katika eneo la Gikomba, Ruto, bila kutaja majina, alimkemea Uhuru kwa kulaumu vita vya Ukraine na Urusi kwa gharama ya juu ya maisha.

"Ati bei ya unga imeenda juu kwa sababu ya vita kule Ukraine? Si vita inaendelea bado Ukraine? Si leo wamesema watateremsha bei ya unga? Kumaanisha ile walikuwa wanatuambia eti mambo ya Ukraine ilikuwa tu ni kutuhadaa," Ruto alisema.

Matamshi hayo yanajiri miezi kadhaa baada ya Rais Uhuru kusema gharama ya juu ya maisha imechangiwa pakubwa na mambo ya nje, ikiwemo vita vya Ukraine na Urusi.

Hati ya mawasiliano ya ndani iliyotiwa saini na Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Kilimo Francis Owino Jumatatu ilisema Wizara ya kilimo itafadhili bei ya unga wa mahindi unaozalishwa na kuuzwa na wasaga mahindi kwa muda wa wiki nne.

Unga sasa utauzwa kwa Sh100, ukishukishwa kutoka kwa bei ya awali kwa Sh130.

“Bei ya reja reja inayopendekezwa ya unga isizidi Sh100 kwa pakiti ya kilo 2, Sh250 kwa pakiti ya kilo 5 na Sh490 kwa pakiti ya kilo 10,” waraka huo ulisomeka.

Ruto alidai kuwa Serikali imepunguza bei hizo kama hatua ya kuwahadaa wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.

"Tutachukua unga lakini tutapiga kura tukiwa na mpango wa kuhakikisha kuwa kila Mkenya ana chakula," alisema.

"Wakenya tayari wameamua... ikiwa utapunguza bei au la, utarejea nyumbani Agosti 9."

Wakati wa kampeni zake, Ruto alilaumu handshake ya 2018 kati ya Uhuru na Raila kwa gharama ya juu ya maisha.

“Mnamo 2018, pakiti ya kilo 2 ya unga wa mahindi iligharimu Sh75. Sasa inauzwa kwa Sh250 na tunaambiwa kwamba baada ya kupigwa kiwiko, [ni] yule jamaa wa Azimio,” alisema wakati wa ziara ya kampeni mjini Kilifi mnamo Juni 26.

(Utafsiri: Samuel Maina)