Wajackoyah avunja kimya kuhusu madai ya kumuidhinisha Raila kuwa rais

Roots Party kimesema video inayosambazwa imefanyiwa ukarabati na kusisitiza kuwa Wajackoyah atakuwa debeni.

Muhtasari

•Roots Party imesema video inayosambazwa imefanyiwa ukarabati na kusisitiza kuwa Wajackoyah atakuwa kwenye debe mnamo Agosti 9.

•Chama hicho kimewahakikishia wafuasi wake kuhusu ushindi katika uchaguzi mkuu ambao umebakisha siku chache kufanyika.

Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Image: The star

Chama cha Roots Party kimepuuzilia mbali madai kuwa mgombea urais wake Profesa George Wajackoyah amemuidhinisha kinara wa ODM Raila Odinga kuwa rais.

Jumatano asubuhi video iliyomuonyesha Wajackoyah akimuidhinisha Raila katika eneo la burudani ilisambazwa sana mitandaoni.

Chama cha Roots  kupitia msemaji wake Wlison Muirani almaarufu Jaymo ule Msee hata hivyo kimesema video inayosambazwa imefanyiwa ukarabati na kusisitiza kuwa Wajackoyah atakuwa kwenye debe mnamo Agosti 9.

"Tungependa kueleza kinaga ubaga kuwa tuna mgombea urais ambaye yuko kwenye debe na atashinda uchaguzi huu. Hatujaidhinisha mgombea mwingine yeyote!" Taarifa iliyotolewa na Jaymo Ule Msee Jumatano asubuhi ilisoma.

Jaymo aliongezea kwa kusema, "Dhana ya kwamba Prof Wajackoyah ameidhinisha Raila Odinga ni mawazo yasiyo na matumaini na ni matamanio ambayo yanapatikana tu akilini mwa vyombo vya habari vyenye upendeleo."

Chama hicho kilibainisha kuwa baadhi ya washindani wao wazamia kwenye mbinu mbaya baada ya kupatwa na wasiwasi kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Aidha kimewahakikishia wafuasi wake kuhusu ushindi katika uchaguzi mkuu ambao umebakisha chini ya wiki moja kufanyika.

Katika video iiliyoenezwa na wanamitandao na baadhi ya vyombo vya habari, Wajackoyah alisikika akimsifu mgombeaji urais wa Azimio la Umoja-One Kenya  Raila Odinga kama mkombozi wa Kenya.

Kiongozi huyo wa Roots Party anasikika akimpa Raila sifa kwa kuhamasisha safari yake ya kuwa  mkombozi.

"Niko hapa kujiunga na kundi la wakombozi katika nchi hii. Mtu ninayemtazama, anayenifanya nisimame hapa si mwingine bali ni Raila Amollo Odinga," Wajackoyah anadaiwa kusema.

Mgombea urais huyo anadaiwa kutoa matamshi hayo wakati akiwahututia wafuasi wake katika eneo moja la burudani  jijini Nairobi.

Haya yanajiri huku zikiwa zimesalia siku sita tu kwa uchaguzi mkuu kufanyika hapa nchini.

Wagombea wanne wakiwemo Raila Odinga, William Ruto, George Wajackoyah na Waihiga Mwaure watamenyana katika kinyang'anyiro cha urais.