IEBC: Zaidi ya Wakenya 6M wamepiga kura kufikia saa sita mchana,chaguzi zikiahirishwa baadhi ya sehemu

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 30.66 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Muhtasari

• Idadi hiyo ni sawa na asilimia 30.66 ya wapiga kura waliojiandikisha.

Wakazi wa Gafuru eneo bunge la Galole, Kaunti ya Tana River wakipiga kura chini ya mti Agosti 9,2022.
Wakazi wa Gafuru eneo bunge la Galole, Kaunti ya Tana River wakipiga kura chini ya mti Agosti 9,2022.
Image: Alphonce Gari

Takriban wapiga kura 6,567,869 wamejitokeza kupiga kura, naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera alisema katika sasisho saa sita mchana.

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Juliana Cherara alifichua kwamba idadi hiyo ni takriban asilimia 30.66, kutoka kwa jumla ya wapigakura milioni 22.1 waliosajiliwa.

Katika muhtasari wa mchana ambao ulitolewa na kaimu huyo mwenyekiti, IEBC ilisema upigaji kura katika nchi za nje zikiwemo zile za mataifa kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika Kusini, Uingereza, Canada, Marekani, Qatar na Ujerumani, mataifa hayo yataandaa uchaguzi ndani ya muda hitajika majira ya nchi hizo.

"Itafanyika kuanzia saa kumi na mbili asubuhi na kukamilika majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa zao kaam ilivyo kawaida," Juliana Cherara alisema.

Tume hiyo pia ilitangaza kuwa upigaji kura umesitishwa katika maeneo ya Kitui Vijijini na Rongai kutokana na mkanganyiko wa karatasi za kupigia kura, siku moja tu baada ya kutoa taarifa za usitishwaji wa chaguzi za ugavana Mombasa na Kakamega pamoja na ubunge baadhi ya sehemu huko Pokot.

Upigaji kura pia umesitishwa huko Eldas kufuatia hali tete iliyoathiri usambazaji wa vifaa katika eneo bunge hilo, baada ya usiku wa kuamkia Jumanne video kusambazwa ikionesha watu wakikimbilia maisha yao kufuatia milio ya bunduki iliyosikika katika ukumbi wa CDF wa Eldas ambao ulikuwa umetengwa kutumika kama kituo cha kuhesabia kura.

"Wakati wa milio ya risasi, maafisa wa uchaguzi walibaki wamenaswa. Uchaguzi umeahirishwa na suala hilo linapaswa kutatuliwa," Cherara aliongeza.

Awali katika kaunti ya Kisii eneo bunge la Bonchari, hali ilikuwa tete baada ya mtu aliyekuwa amejihami na bunduki na ambaye baadae alitajwa kuwa mmoja wa maafisa wa polisi aliyevalia raia kumpiga risasi mtu mmoja kwa tumbo katika kile kilitajwa kuwa tofauti za kisiasa baina yao. Hali hiyo ilisababisha maandamano makali ambayo yalitatiza shughuli za kawaida kufanyika kwa uchaguzi.

Kwingineko katika maeneo ya Matungu, mgombea urais wakili msomi profesa George Wajackoyah alizua vikali baada ya mtambo wa KIEMS kukwama kuwatambua wapiga kura katika maeneo mengi kaunti ya Kakamega ila baada ya Subira ya kitambo kidogo, mgombea huyo aliweza kupiga kura kabla ya kuzungumza na wanahabari huku akionekana kumtuhumu mwenyekiti wa IEBC kwa kutoweka mipango Madhubuti ya kuhakikisha kwamba sajili mbadala iliyochapishwa ilikuwepo kama sajili ya kidijitali ingefeli.