Wajackoyah ashindwa kupiga kura mtambo wa KIEMS ukifeli

Wajackoyah alikuwa anatarajia kupiga kura eneo la Matungu.

Muhtasari

• Mtambo wa kidijitali wa KIEMS ulifeli kuwatambua wapiga kura wote akiwemo yeye.

Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Image: The star

Mgombea urais wa chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah ameshindwa kupiga kura katika kituo cha Matungu baada ya ya mtambo wa kidijitali wa KIEMS  kufeli kuwatambua wapiga kura akiwemo yeye.

Maafisa wa uchaguzi katika kituo hicho waliwataka wapiga kura kusubiri zaidi ili kujaribu kulitatua tatizo hilo na Wajackoyah alipoulizwa na waandishi wa habari maoni yake kuhusu hilo, alidinda kulizungumzia na kusema kwamba atazungumza baada ya hatima ya mtambo huo wa KIEMS.

Kushindwa kwa vifaa vya KIEMs kuliripotiwa katika vituo vingine vingi vya kupigia kura katika eneo bunge la Matungu.

Upigaji kura ulicheleweshwa kwa zaidi ya saa nne katika vituo vya Namulungu, Mirere na Namanga na Khalaba kutokana na kushindwa kwa vifaa vya KIEMs.

Wapiga kura waliokuwa na wasiwasi waliwashirikisha maafisa wa uchaguzi katika mabadilishano makali wakidai kuwa hiyo ni sehemu ya mipango ya wizi.

Afisa Uchaguzi (RO) wa kaunti ya Kakamega Joseph Ayata alisema kuwa timu ya kiufundi ya tume hiyo ilikuwa ikifanya kazi kutatua suala hilo.

Alisema ni tatizo la kiufundi na halina uhusiano wowote na uchakachuaji wa mchakato wa upigaji kura.