ODM Yashindwa Kupata Kiti cha Ubunge Kisumu East Kwa Mara ya Pili Mfululizo

Shakeel Shabbir aliibuka mshindi kwa kujizolea takribani kura 35,704 huku akiwa mgombea huru asiyetegemea chama chochote.

Muhtasari

• Shabbir alimshinda Oricho wa ODM kwa mara ya pili mfululizo katika chaguzi za 2017 na huu wa sasa wa 2022.

Mbunge mteule wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir wa Independent akionyesha cheti chake baada ya kupata kura 35,704 dhidi ya Nicholas Oricho wa ODM, aliyeibuka wa pili kwa kura 28,491, katika Shule ya Sekondari ya Kasagam mnamo Agosti 11, 2022.
Mbunge mteule wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir wa Independent akionyesha cheti chake baada ya kupata kura 35,704 dhidi ya Nicholas Oricho wa ODM, aliyeibuka wa pili kwa kura 28,491, katika Shule ya Sekondari ya Kasagam mnamo Agosti 11, 2022.
Image: DANIEL OGENDO

Kwa mara ya pili mtawalia, chama cha ODM kimeshindwa kushinda kiti cha ubunge katika kitivo chake cha nyumbani kabisa, eneo bunge la Kisumu Mashariki.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika eneo bunge hilo Alhamis asubuhi alitangaza mshindi katika uchaguzi ambao umefanyika hivi majuzi ambapi kwa mara nyingine tena, Shakeel Shabbir aliibuka mshindi kwa kujizolea takribani kura 35,704 huku akiwa mgombea huru asiyetegemea chama chochote.

Shabbir ambaye ni mbunge wa sasa wa eneo hilo pia katika uchaguzi mkuu wa 2017 alichaguliwa kama mbunge kama mgombea huru baada ya kudai kudhulumiwa katika uchaguzi wa mchujo wa vyama ambapo alikuwa mwanachama wa ODM.

ODM ambacho kinaongozwa na kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kinatajwa kuwa na ufuasi mkubwa katika jiji pana la Kisumu na ndio eneo linalotajwa kuwa nyumbani kwa waasisi wa chama hicho cha chungwa.

Katika uchaguzi huu ambao umekamilika juzi, ODM tena ilikuwa imemuidhinisha Nicolas Oricho katika jaribio la kurudisha kiti cha ubunge Kisumu East chini ya himaya yake ila kwa mara ya pili tena wakashindwa baada ya Shabbir kuibuka mshindi tena.

Shabbir alikuwa mbunge kwa mara ya kwanza eneo bunge hilo mwaka wa 2007, ambapo sasa kutoka eneo pana la Nyanza, anakuwa mbunge wa pekee kubaki ofisini tangia mwaka huo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti hicho, Shabbir alisema mapenzi ya wananchi yameonekana.

"Nimenyenyekea kwa imani iliyoonyeshwa na wapiga kura kwangu. Imesisitiza kuwa wananchi wanapokuwa na imani nanyi, haijalishi mtu anahusishwa na chama gani cha siasa," alisema.