Mpiga kura John Kamau awasilisha kesi mahakama ya upeo kupinga ushindi wa Ruto

Kuwasilishwa kwa kesi hii kunajiri tu siku ambayo pia mawakili wa Azimio wanatarajiwa kuwasilisha kesi yao dhidi ya ushindi wa Ruto

Muhtasari

• Mpiga kura huyo anadai kwamba Ruto na Gachagua hawakuchaguliwa kihalali kama rais na naibu wake mtawalia.

Mahakama ya upeo
Image: Maktaba

Mahakama ya upeo wa juu nchini Kenya Jumatatu asubuhi ilidhibitisha kupokea ombi la kwanza kabisa kutoka kwa mpiga kura kwa jina John Njoroge Kamau ambaye analenga kupinga matokeo ya urais ambayo yalimpa naibu wa rais anayeondoka William Ruto ushindi.

Katika ombi hilo la kutaka mahakama ibatilishe ushindi wa Ruto, makamishna wanne wa IEBC waliojitenga na matokeo hayo wameorodheshwa kama wahusika muhimu watakaotoa Ushahidi dhidi ya matokeo hayo.

Wahusika wengine ambao pia mpiga kura huyo amewataja katika ombi lake ni makamishna wengine wawili waliosalia upande wa mwenyekiti Wafula Chebukati.

Mlalamishi mkuu Raila Odinga na aliyekuwa mgombea mwenza wake Martha Karua pia wametajwa katika orodha ya wale wanaolenga kuhusika katika kesi hiyo ambapo jana muungano wa Azimio la Umoja One Kenya waliweka wazi kuwa Jumatatu leo hii watawasilisha ombi lao rasmi katika mahakama hiyo ili kupinga uamuzi wa IEBC kumtaja Ruto kama rais mteule.

Katika ombi hilo, rais mteule William Ruto, naibu wake Rigathi Gachagua, tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC na mwenyekiti wake Wafula Chebukati wametajwa kama washtakiwa katika kesi hiyo na watahitajika kujibu malalamishi yaliyoibuliwa na mpiga kura huyo.

Bernard Kasavuli ambaye ni naibu msajili wa kesi katika mahakama hiyo ya upeo alisema kwamab mpaka sasa hilo ndilo ombi tu ambalo wamepokea, huku wananchi wakitarajia kusikia kwamba Mawakili wa mrengo wa Azimio kabla ya saa nane adhuhuri watawasilisha ombi lao katika mahakama hiyo pia.

Kamau katika ombi lake anatafuta agizo la kuagiza IEBC kuandaa na kuendesha uchaguzi mpya wa urais. Pia kinachotafutwa ni tamko kwamba Chebukati alitenda dosari za uchaguzi na anapaswa kuchunguzwa kwa uwezekano wa matukio ya uhalifu.

Mpiga kura huyo anadai kwamba Ruto na Gachagua hawakuchaguliwa kihalali kama rais na naibu wake mtawalia.