Raila amfanyia kampeni Abdulswamad mjini Mombasa huku Gachagua akizuru Rongai

Uchaguzi wa ugavana utafanyika katika kaunti za Mombasa na Kakamega na eneo bunge nne

Muhtasari

•Kampeni zinatarajiwa kukamilika Ijumaa jioni kwa mujibu wa kanuni za IEBC zinazobainisha kuwa shughuli zote za kisiasa katika maeneo ya uchaguzi kukoma.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Kinara wa muungano wa Azimio one Kenya Raila Odinga amezuru kaunti ya Mombasa kumpigia debe mgombea wa ODM katika kinyang'anyiro cha ugavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Nassir. 

Raila aliwasili katika mji wa Mombasa na kuandaa mikutano kadhaa na washika dau mbali mbali kwa lengo la kumpiga jeki mgombea wa chama chake. 

Kiongozi huyo wa Azimio alikutana na viongozi wa mashinani na baadaye kufanya ziara ya kukutana na wananchi.

Uchaguzi wa kutafuta gavana wa Mombasa uliahirishwa na umepangiwa kufanyika Jumatatu wiki ijayo.

Kwingineko, Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua na Gavana Mteule wa Nakuru Susan Kihiki wanaongoza kampeni za mgombea wa UDA katika eneo bunge la Rongai, kiti hicho kinashikiliwa na Raymond Moi wa chama cha KANU. 

"Baada ya kufanikiwa kuwakomboa wenyeji wa Mlima Kenya kutoka katika utumwa wa familia moja, mashujaa hao wa Mlima Kenya wanaelekea eneo bunge la Rongai, kaunti ya Nakuru kusaidia kuwakomboa wakazi wa Rongai kutoka katika utumwa wa familia nyingine," Gachagua alisema kwenye ukurasa wake wa twitter.

Seneta Mteule wa Kakamega Boni Khalwale anaongoza kampeni za Kenya Kwanza kupigia debe Cleophas Malala ambaye ni miongoni mwa wagombeaji wanaotaka kuchukua nafasi ya Gavana anayeondoka Wycliffe Oparanya.

Kampeni zinatarajiwa kukamilika Ijumaa jioni kwa mujibu wa kanuni za IEBC .

Uchaguzi wa ugavana utafanyika katika kaunti za Mombasa na Kakamega na maeneo bunge manne ya Pokot Kusini, Kitui Rural, Rongai na Kacheliba.