Siwezi kujiuzulu chamani mpaka Wajackoyah mwenyewe anitupe nje - Justina Wamae

Alisema Wajackoyah alijaribu kumtamausha ili ajiuzulu ila akashindwa

Muhtasari

• Mimi bado ni mwanachama kwa sababu sijapewa barua ya kufurushwa. - Wamae.

Viongozi wa chama cha Roots.
JUSTINA WAMAE, GEORGE WAJACKOYAH Viongozi wa chama cha Roots.
Image: Maktaba

Justina Wamae, aliyekuwa mgombea mwenza wa urais wa wakili msomi George Wajackoyah katika chama cha Roots ametenganisha ngano na makapi kwa kubainisha kwamba yeye bado ni mwanachama wa Roots.

Maneno ya Wamae yanakuja siku moja tu baada ya uvumi kuzuka kwamba Wajackoyah amemtema Wamae chamani na kumteua mtu mwingine kuwa naibu mwenyekiti wa chama.

Akizungumza katika kipindi cha YouTube cha Gerald Bitok, Wamae alisisitiza kwamba yeye bado ni mwanachana na pia ndiye naibu mwenyekiti halali. Alisema kwamba licha ya shinikizo kutoka kwa kiongozi wa chama, hana nia yoyote ya kung’atuka mpaka pale atakapong’atuliwa kwa nguvu.

“Mimi tayari ni mwanachama wa Roots. Nitazidi kuwa mwanachama kwa sababu sijajiuzulu. Bado ninasubiri barua ya kufurushwa. Siwezi kujiuzulu mpaka pale Wajackoyah atanitupa nje," Wamae aliweka wazi msimamo wake.

Akitoa sababu ya kutojiuzulu, Wamae alisema kwamba nchini Kenya watu hawajafikia kiwango cha kuelewa mtu wakati anapofanya uamuzi wa kuachia ngazi.

Alisema kwamba hata Martha Karua kipindi akihudumu kweney serikali ya hayati rais Kibaki alijiuzulu lakini watu hawakumuelewa licha ya kusema kwamba zilikuwa tofauti za utendakazi. Pia alisema hata Polycarp Igathe alipoachia ngazi kama naibu gavana Nairobi, wengi walimkosoa vikali na hiyo ndio sababu yake kukwamilia mpaka ang’atuliwe kwa nguvu.

“Mimi naelewa Wakenya, maisha yetu ni kung’ang’ana katika nchi hii kuhangaika kutafuta pesa. Kwa hiyo wakati unajiuzulu, watu hawawezi kuelewa kama Mkenya. Sasa mimi nilichokisema ni kwamba kwa sababu kutofautiana kwangu naye kulikuwa juu ya misimamo, na kiongozi wa chama amesema anamiliki chama, mimi nilimuacha afanye vile anataka,” Wamae alisema.

Pia alifunguka makubwa kwamba ni ukweli jinsi mrengo wa vijana katika chama hicho walivyodai kwamba kiongozi wa chama profesa Wajackoyah alikuwa anamfanyia figisu na mapicha picha ili atamauke na kuachia ngazi.

“Alikuwa anajaribu tu kunitamausha ili nijiuzulu ili aweze kumpa nafasi hiyo mtu mwingine. Ila anafaa kujua kwamab mimi siwezi kujiuzulu mpaka anitoe mwenyewe,” Wamae alisema bila kutetereka.

Alisisitiza kwamba yeye hakuwa kabisa mradi kwa sababu hakutaka kusaliti uaminifu ambao Wakenya waliuweka kwao.