Hatuwezi kupanda jukwaa moja!- Muthama azungumzia ugomvi wake na gavana Mutua

Muhtasari

•Muthama alikiri kwamba amekuwa akizozana na gavana huyo wa muhula wa pili katika kipindi cha takriban miaka tisa ambacho kimepita kuhusiana na masuala ya uongozi.

•Alithibitisha kuwa mzozo wao ndio ulifanya akose kuhudhuria mkutano wa Kenya Kwanza uliofanyika mjini Tala siku ya Jumanne.

Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama wakati wa mkutano na wanahabari katika ofisi yake ya Gigiri siku ya Jumatatu.
Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama wakati wa mkutano na wanahabari katika ofisi yake ya Gigiri siku ya Jumatatu.
Image: MERCY MUMO

Mwenyekiti wa UDA Johnstone Muthama ameweka wazi kuwa hayupo tayari kufanya kuwa kwenye jukwaa moja na gavana Alfred Mutua licha ya yeye pamoja na chama chake cha Maendeleo Chap Chap kujiunga na Muungano wa Kenya Kwanza.

Akiwa kwenye mahojiano na KTN News, Muthama alikiri kwamba amekuwa akizozana na gavana huyo wa muhula wa pili katika kipindi cha takriban miaka tisa ambacho kimepita kuhusiana na masuala ya uongozi.

"Mimi na Mutua tuna matatizo na sio shida za kibinafsi, ni shida za kinafsi, ni shida za uongozi. Katika kipindi cha miaka tisa na miezi tisa sasa, ikiwa imebaki miezi mitatu tu itimie miaka 10, nimekuwa na shida sana na gavana Mutua," Muthama alisema.

Seneta huyo wa zamani wa Machakos amemshtumu Mutua kwa kuwahadaa wakazi wa kaunti hiyo kuhusu masuala ya maendeleo. Alisema gavana huyo alidanganya kuhusu suala la kusuluhisha tatizo la maji, kusaidia wakulima na kuimarisha usalama katika kaunti ya Machakos.

Muthama amesema ujio wa Mutua katika Muungano wa Kenya Kwanza hautafanya azike mzozo wao katika kaburi la sahau. Alithibitisha kuwa mzozo wao ndio ulifanya akose kuhudhuria mkutano wa Kenya Kwanza uliofanyika mjini Tala siku ya Jumanne.

"Ni ngumu sana kuwa marafiki na Mutua eti kwa sababu amekuja kujiunga na Kenya Kwanza baada ya miaka tisa na miezi tisa ya kuvurugana naye nikisema hafanyi kazi vizuri. Niliona msimamo wangu, roho yangu na imani haiwezi kunipeleka kwa mkutano ule," Alisema.

Alisema amani kati yao itapatikana pindi tu gavana Mutua atakapokubali kuomba msamaha hadharani mbele ya wakazi wa Machakos.

"Sina shida na Mutua kama mtu binafsi. Sina shida na chama cha Maendeleo Chap Chap. Mutua amfanyie naibu rais kampeni, afanye kampeni zake, ata mimi anipigie kura yake. Lakini sibaduki kuwa Mutua ni mhuni, ni muongo, ni mtu asiyeamini. Amedanganya na kutesa watu wa Machakos," Alisema

Muthama hata hivyo aliweka wazi kuwa alihusika katika suala la gavana huyo kutia saini mkataba na Kenya Kwanza.