Kalonzo, Mbadi wapendekezwa kuwa spika bungeni

Orero alibainisha kuwa watamuunga mkono mtu ambaye muungano huo utachagua.

Muhtasari

•Orero alidokeza kuwa wawili hao walikuwa wamependekezwa na wanachama wa muungano wa Azimio-One Kenya.

•Alidokeza kuwa Azimio itateua wagombea uspika katika siku zijazo na kueleza kuwa sasa kipaumbele chao ni kesi  ya urais.

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua
Image: TWITTER// MARTHA KARUA

Mbunge mteule wa Kibra Peter Orero amedokeza kuwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa mbunge wa Suba Kusini John Mbadi wamependekezwa kuchukua wadhifa wa Spika wa Bunge la Kitaifa.

Katika mahojiano na Ramogi TV,  Mwalimu huyo mkuu wa zamani wa  Upper Hill alidokeza kuwa wawili hao walikuwa wamependekezwa na wanachama wa muungano wa Azimio-One Kenya.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa Kalonzo na Mbadi bado hawajaonyeha nia ya kugombea wadhifa huo. Alibainisha kuwa watamuunga mkono mtu ambaye muungano huo utachagua kwani wote wamehitimu.

“Mbadi ni rafiki yangu na tulipokutana hakuniambia anataka kuwa spika, ikiwa wabunge wanadhani yeye ndiye bora kwa nafasi hiyo basi tutamuunga mkono. Jina la Kalonzo pia ilitajwa, ikitokea atatangaza kuwa anataka nafasi hiyo, tutamuunga mkono pia," Orero alisema.

Aliongeza kuwa muungano huo unaongozwa na Raila Odinga utateua wagombea wa nafasi hiyo katika siku zijazo na kubainisha kuwa kwa sasa kipaumbele chao ni kesi  ya urais lililowasilishwa katika Mahakama ya Juu.

Azimio inatazamia kuwashawishi wabunge waliochaguliwa katika Bunge la Kitaifa ili kuchukua nafasi ya maspika.

Hata hivyo, wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Kenya Kwanza ambayo unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Kenya Kwanza kwa upande  wake ulionekana kumuunga mkono Seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuwania nafasi hiyo.