Patanisho: Mwanadada awapatia wanaume simu wamtukane mumewe baada ya kulewa

Oyugi alidai kuwa mkewe alikuwa na tabia ya ulevi na kutoka nje ya ndoa.

Muhtasari

•Oyugi alisema kuwa ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika kufuatia tabia mbaya za mke wake. 

•Frida alifichua kwamba yeye ndiye aliyemkaribisha Oyugi nyumbani kwake na alikuwa akilipa kodi.

Gidi
Image: RADIO JAMBO

Charles Oyugi (28) kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Fridah (29)  ambaye walikosana naye wiki mbili zilizopita.

Oyugi alisema kuwa ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika kufuatia tabia mbaya za mke wake. Alidai kuwa mkewe alikuwa na tabia ya ulevi na kutoka nje ya ndoa.

"Nikitoka kwa nyumba alikuwa akitoka nyuma yangu anaenda kukunywa.Nikimuuliza alikuwa akiniambia kuwa mimi ni mjinga. Mimi mwenyewe sikunywi pombe. Akifanya makosa hataki kuulizwa maswali," alisema.

Oyugi alifichua kuwa alimuoa Bi Frida tayari akiwa na watoto wawili wasichana. Wawili hao hawana mtoto pamoja.

Alibainisha kuwa mkewe hakutaka kuulizwa maswali yoyote licha ya kuwa mkosaji wa mara kwa mara.

"Wakati akienda kukunywa alikuwa anapatia wanaume simu ili wanitusi. Akirudi alafu nimuulize mbona alikuwa akipatiana simu anasema kwamba sio yeye. Nataka tu kujua kama tunaweza kurudiana," alisema.

Oyugi alisema kwamba ana matumaini kuwa Bi Frida anaweza kurekebisha tabia zake iwapo watarudiana.

"Tulikuwa tunafanya kazi sawa. Mimi ndiye nilikuwa nalipa kodi. Baada ya kutengana naye sijakuwa nikilipa. Mimi nilitoka huko nikamuchia nyumba nikaenda kupanga kwingine," alisema.

Fridah alipopigiwa simu alifichua makosa mengi ya Oyugi ambayo hakuwa amesema katika maelezo yake.

"Alifichua kuwa Oyugi hajawahi kumpeleka kwao wala kumtambulisha kwa wazazi wake. Pia alifichua kwamba Oyugi alichukua pikipiki kwa mkopo ambapo alimsimamia ila baadae akashindwa kulipa. Wakati ulitoa tracker akazima simu, ulitaka mimi nishikwe, hiyo ni sawa kweli," alisema.

Aidha, alifichua kwamba yeye ndiye aliyemkaribisha Oyugi nyumbani kwake na alikuwa akilipa kodi.

"Oyugi alikuja kwangu tukakaa kwangu . Hajanioa tukaishi kwake. Alikuja kwangu tukakaa," alisema.

Frida hakukubali kurudiana na Oyugi wala kutupilia mbali uwezekano wa wao kurudiana na badala yake akamshauri apige hatua ya kuandaa kikao na familia ili waweze kutafuta suluhu ya mzozo wao.