King Kaka ahamia Arsenal kufuatia 'uhusiano wa kidhuluma' na Mashetani Wekundu

Muhtasari

•King Kaka ameeleza kutoridhishwa kwake na matokeo hafifu ambayo timu hiyo imekuwa ikiandikisha katika mechi za hivi majuzi.

•Hatua ya King Kaka ilijiri muda mfupi baada ya Mashetani Wekundu kupokea kichapo cha 4-1 kutoka kwa majirani wao Manchester City. 

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki Kennedy Ombima almaarufu King Kaka ametangaza rasmi kuwa kuanzia sasa atakuwa anashabikia timu ya Arsenal.

Kupitia kanda ya video ambayo alipakia Instagram, King Kaka ambaye kwa miaka mingi amekuwa akishabikia Manchester United ameeleza kutoridhishwa kwake na matokeo hafifu ambayo timu hiyo imekuwa ikiandikisha katika mechi za hivi majuzi.

Rapa huyo amesema aliafikia hatua ya kugura United baada ya uhusiano wake na klabu hiyo kuanza kuwa sumu huku akieleza kuwa tayari ameanza kufurahia matunda ya uhusiano wake mpya na 'The Gunners'.

"Kama wengi wenu mnavyojua, nimekuwa katika uhusiano. Uhusiano huo ulianza kuwa sumu, sijakuwa na raha. Nadhani ni wakati murwa nianze kutafuta  raha kwingineko. Nimeanza kupata zawadi kutoka kwa uhusiano wangu mpya. Bidii ambayo uhusiano huo unaweka umefanya nione kuwa kuna  matunda mazuri zaidi. Najitokeza hadharani kutangaza wazi kwamba kwa sasa niko katika uhusiano mpya na najua nitakuwa na raha. Raha sio hakikisho lakini tutafanya ifanye kazi. Ni rasmi kwamba sasa nashabikia Arsenal," King Kaka alisema.

Hatua hii ya King Kaka ilijiri muda mfupi baada ya Mashetani Wekundu kupokea kichapo cha 4-1 kutoka kwa majirani wao Manchester City. Wanabunduki kwa upande wao walipata ushindi wa 3-2 ugenini dhidi ya Watford.

King Kaka amekuwa shabiki sugu wa United kwa muda mrefu ilhali mkewe Nana Owiti amekuwa akiishabikia Arsenal.