Mwanadada awabwaga wanaume kwenye shindano la kula

Mwanamke alionekana kuchukua dakika chache mno kuwashinda wanaume hao.

Muhtasari

• Shindano hilo la ulaji lilikuwa katika tamasha za Emure yam la 2022.

@ekititrends
@ekititrends
Image: Twitter

Mwanamke mmoja aligeuka gumzo la siku baada ya kuwabwaga wanaume kwenye shindano la ulaji nchini kwenye finali kuu ya tamasha hizo za Emure yam la 2022.

Shindano hilo lilikuwa na wanaume wengi zaidi waliokuwa wakionyesha ustadi wao wa kula huku mwanadada huyo akichukua dakika kidogo sana kumaliza milima ya chakula kwa minajili ya kupata tuzo.

Mwanamke huyo alionekana akibugia na kujikaza kumaliza chakula hicho kabla wenzake katika shindano hilo lililokuwa limehudhuriwa na watu wengi mno.

Watu waliokuwa wamehudhuria tamasha hizo na kushuhudia shindano hilo walimshabikia mwanamke huyo kwa kuibuka wa kwanza kwenye kinyang'anyiro hicho.

Wakiwa wamevalia mavazi ya kienyeji, washiriki waliketi kwa duara kwenye sakafu walipokuwa wakiharakisha kumeza bila kutafuna mlo huo ulioandaliwa kwa ajili ya mashindano.

Video hiyo iliyopakiwa kwenye mtandao wa Twitter iliacha wanamitandao wakiwa wamepigwa na butwaa kwani ni nadra sana kwa mwanamke kuonekana kwenye michezo ya aina hiyo.

Wanamitandao wengi kwenye mtandao huo walionekana kutoa msururu wa jumbe kali huku wakiitikia ushindi wa mwanadada huyo kwa mawazo ya kuchekesha.

 "Siamini mwanadada ameshinda. Niliona kama hatamaliza. Anavyokula viazi vikuu vilivyopondwa, kunywa supu na kubugia kibuyu cha mvinyo ni kitu kinachostukiza."  @fingertrickz alisema.

''Ikiwa nitawahi kushiriki katika mchezo kama huu,nitachukua muda wangu tu kwa sababu najua siwezi kushinda, labda nibebe chakula nikale nyumbani'' Swagger Shiggo alisema.

''Nawaza kama hawa wasichana watalala na kuamka asubuhi'' @ziinnab22 alionyesha kuwajari.