"Namheshimu sana mpenzi wake" Mulamwah azungumzia uhusiano na 'bestie' wake, Ruth

Mulamwah aliweka wazi kuwa hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yake na Ruth.

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alisema kwamba mpenzi wa Ruth ni rafiki yake mkubwa na hana tatizo lolote na urafiki wao.

•Alisema huwa anakutana mara kwa mara na mwanaume huyo na kushiriki mazungumzo ya kirafiki.

Mulamwah na bestie wake Ruth K
Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji mashuhuri David Oyando almaarufu Mulamwah amebainisha kuwa uhusiano wake na 'bestie' wake Ruth K ni wa kirafiki tu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mpenzi huyo wa zamani wa Carrol Sonnie aliweka wazi kuwa hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yake na muigizaji huyo.

"Hakuna uhusiano ya kimapenzi kusema kweli. Namheshimu sana mpenzi wake. Ako na mpenzi," mchekeshaji huyo alisema.

Baba huyo wa binti mmoja alisema kwamba mpenzi wa Ruth ni rafiki yake mkubwa na hana tatizo lolote na urafiki wao.

Alifichua kwamba huwa anakutana mara kwa mara na mwanaume huyo na kushiriki mazungumzo ya kirafiki.

"Huwa tunakutana. Ni rafiki yangu. Hananga maneno, anaelewa hii biashara," alisema.

Siku ya Jumanne wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya Wapendanao, wawili hao waliongeza kuni kwenye moto wa tetesi za mahusiano baina yao baada ya kuchapisha picha na video za kutiliwa shaka.

Video moja ambayo Mulamwah alichapisha kwenye Instagram iliwaonyesha wakikumbatiana na kubusu kama wapenzi.

"Kheri ya siku ya Valentines bestie ❤❤ @ruth_k," aliandika chini ya video hiyo.

Ruth kwa upande wake alimsherehekea mchekeshaji huyo na kumweleza jinsi anavyofurahia kila dakika anayotumia naye.

"Kila wakati ninatumia nawe nauthamini, kicheko, kumbukumbu nzuri na machozi yaliyomwagika katika siku hizo za giza. Kukutaza ukishinda maishani ni maombi yaliyojibiwa. Kwa mtu jasiri zaidi na mwenye upendo zaidi ninayejua, kheri ya siku ya wapendanao. Nitakuchagua kila wakati nikiagizwa kufanya hivyo. Besties hadi milele❤❤ @mulamwah," Ruth alimwandikia Mulamwah siku ya Jumanne.

Mwezi uliopita, mzazi mwenza huyo wa Carrol Sonnie alisema kuwa Ruth amekuwa rafiki yake mkubwa tangu utotoni.

"Rafiki yangu mzuri sana tangu utotoni @ruthk,” aliandika chini ya picha nzuri za muigizaji huyo ambayo alizochapisha.

Hata hivyo, mchekeshaji huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu jinsi walivyokutana na jinsi safari yao ya urafiki imekuwa.

Ruth alijibu chapisho la baba huyo wa binti mmoja na alionekana kuunga mkono maelezo ambayo alitoa kwenye picha.

"Tumetoka mbali 😍😍 Kwa miaka mingi mingine ❤," alisema.

Kwa muda sasa mrefu, Wakenya wamekuwa wakihoji sana kuhusu uhusiano halisi kati ya mchekeshaji huyo na Ruth hasa kutokana na ukaribu wao na matendo yao pamoja kwenye mitandao ya kijamii.

Wawili hao wameonekana kuwa na ukaribu mkubwa tangu Ruth asainiwe katika lebo ya Mulamwah Entertainment. Mara nyingi wameonekana pamoja kwenye hafla maalum na wamekuwa wakiitana 'bestie'.

Baada ya kutengana na Carrol Sonnie mwaka wa 2021, Mulamwah alikuwa amemtambulisha Ruth kama mpenzi wake.

Mnamo mwezi Machi mwaka jana hata hivyo, mchekeshaji huyo alisema hachumbiani na yeyote na akadai kwamba hakuna uhusiano wowote wa kimapenzi kati yake na Ruth kama ilivyokuwa ikiaminika wakati huo.

Wakati huo, alimtambulisha kipusa huyo kama msanii wake mpya katika lebo yake, 'Mulamwah Ent' na kuongeza kwamba hawakuwahi kuwa wapenzi na  hawakuwa na mpango wa kuchumbiana siku za usoni.

"Kusema kweli hatujawahi kuchumbiana , na hatuna nia ya kuchumbiana.Haikueleweka. Kwa upande wangu mimi nabaki single na kuzingatia kazi zangu na miradi mingine iliyo mbele yangu," alisema.