Killy na Cheed washauriwa kurudi kwa Alikiba baada ya kutemwa na Harmonize

Killy na Cheed walikuwa kwenye lebo ya Kings Music kabla ya kujiunga na Konde Music WorldWide

Muhtasari

• Hivi majuzi, mkataba wao na lebo ya Harmonize ya Konde Music WorldWide ulikatizwa ila hawakufurahia jambo hilo.

Chawa wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Baba Levo aliwashauri wanamuziki Killy na Cheed kumwomba radhi Alikiba ili warudi kwenye lebo yake ya Kings Music.

Katika mahojiano yake na SimuliziNa Sauti, Levo alisema kuwa anawaaminia wasanii hao wawili kuwa na kipaji kikubwa na kuwa wanaweza wakakuza sanaa yao zaidi.

Alisema kwamba aliamini kuwa Alikiba ana uwezo wa kuwasaidia Killy na Cheed katika muziki wao na kuwa ana pesa za kutosha kuwasimamia wawili hao bila utatanishi wowote wala kuwa na majuto baadaye.

"Warudi kule walikotokea ,King Kiba tayari ni mtu mkubwa kwa hivyo na naamini kuwa watafanya vizuri kwani walikuwa washaanza kufanya vizuri ila labda walishikwa na tamaa ya kuenda kwa Harmonize," alisema.

Aliongeza kuwa matumizi ya wasanii hao wawili ni makubwa na kuna uwezekano kuwa kipato walichokuwa wakipata kwenye lebo ya Harmonize kilikuwa kidogo.

Alisema alifahamu kuwa  Harmonize angeshindwa kuwasimamia wanamuziki hao wawili katika lebo yake.

"Nimeona Diamond alivyotumia hela kwa Zuchu, zaidi ya milioni tatu au nne,ukilipa milioni tano kisha uje ulie baadaye ina maana kuwa huna,nilijua kuwa atashindwa," alisema.

Aliwashauri wasanii kujipanga na kuwa sawa kifedha kabla ya kuwa na lebo kwani kusimamia wasanii wengine kunahitaji hela.

Alisema, kuwa na kipaji pekee hakuwezi kuwafanya wasanii kuwasimamia wasanii wengine wadogo wanaokua na kuwa inataka hela .

Hii ni baada ya mkataba wa Killy na Cheed wa miaka kumi katika lebo ya Harmonize ya Konde Music Worlwide kusimamishwa.

Baada ya mkataba huo kusimamishwa, wanamuziki hao wawili walienda kwenye bodi ya sanaa ya nchini humo,  BASATA na kulalamika kuwa mkataba wao wa miaka kumi ulikatizwa na Harmonize bila haki.

Walisema kuwa waliingia kwenye Lebo ya konde music kwa maandishi ila mkataba ulipovunjwa hakuna barua yoyote ya maandishi iliyowasilishwa kwao.