Nimeridhika na mabinti wangu! Wahu ajibu shinikizo la kupata mtoto wa kiume

Mke huyo wa Nameless alisema kuwa anafurahia kuwa mama ya watoto wa kike.

Muhtasari

•Alikuwa anamjibu shabiki yake mmoja aliyemuuliza kama alikuwa na azimio la kupata mtoto wa kiume.

•Wahu alisema, "Sina haja ya kumtafuta mtoto wa kiume hata kamwe... Nina furaha na nimeridhika na mabinti wangu," 

Mwanamuziki Wahu Kagwi ameweka wazi kuwa hayuko chini ya shinikizo la kupata mtoto wa kiume kwani watoto wake wa kike wamemtosha.

Amesema kuwa ana furaha kuwa mama ya watoto wa kike na kuwa suala la kupata mtoto wa kiume ni mpango wa Mungu.

Alikuwa anamjibu shabiki yake mmoja aliyemuuliza kama alikuwa na azimio la kupata mtoto wa kiume.

" Hongera lakini una matumaini ya kupata mtoto wa kiume?" mwanamitandao mmoja aliuliza.

Wahu alimjibu, "Sina haja ya kumtafuta mtoto wa kiume hata kamwe... Nina furaha na nimeridhika na mabinti wangu," 

Wahu na mume wake Nameless wameonekana kuridhika na kuwa na watoto wa kike pekee licha ya baadhi ya mashabiki wao kuwapa shinikizo la kupata mtoto wa kiume.

Wanandoa hao wamedhihirisha kuwa hawajali kuwa na watoto wa  jinsia yeyote na waliweka wazi kuwa Mungu ndiye anayebariki watu na watoto.

Wamejipa majina ya majazi kama #mamagirls na #babagirls kuonyesha jinsi walivyopenda kuwalea mabinti.

Hivi majuzi, mwanamuziki Nameless alimjibu shabiki aliyemshauri kutafuta mtoto wa kiume ili kuliokoa jina lake huko mbelelni.

Nameless alisema kuwa fikra hiyo ya watu ya kuangazia jinsia moja ni fikra ya watu wa zamani ambayo haifai kuwa sasa.

Alisema kuwa hata watu wakiongea bado anawapenda mabinti wake sana na ataendelea kuwalea ipasavyo.

"Kama unanifahamu vyema, unajua kuwa nitapigania mtoto wa kike na nitapigania mtoto wa kiume," Nameless alisema huku akisisitiza kuwa hatetei jinsia moja pekee.

Alimjibu shabiki aliyemwambia atafute mtoto wa kiume na kumwambia kuwa anataka kukumbukwa kama baba ya watoto wa kike watatu .

"Saa nyingine tunajingusha na tamaduni za kitambo ambazo zimepitwa na wakati. Naelewa kuwa tumefundishwa kufuata tamaduni hizo bila kuuliza swali ila tunafaa kuwa na hekima ili tutambue tamaduni ambazo si za haki," Nameless alisema.