Polisi wafurusha watu baada ya lori lingine la mafuta kuanguka Kisumu

Punde baada ya ajali hiyo kutokea maafisa wa usalama walikimbia kwenye eneo la tukio na kufurusha kikundi cha watu kilichokuwa kimejumuika pale

Muhtasari

•Siku chache tu baada tangi la mafuta kulipuka na kuua watu 15 maeneo ya Gem, lori lingine lililokuwa limebeba tangi lenye zaidi ya lita 30,000 za mafuta linaripotiwa kupoteza mwelekeo kwenye barabara ya kutoka Kisumu kuelekea Kondele na kuanguka ndani ya shimo maeneo ya Kasagam jioni ya Jumatatu.

Image: FAITH MATETE

Siku chache tu baada tangi la mafuta kulipuka na kuua watu 15 maeneo ya Gem, lori lingine lililokuwa limebeba tangi lenye zaidi ya lita 30,000 za mafuta linaripotiwa kupoteza mwelekeo kwenye barabara ya kutoka Kisumu kuelekea Kondele na kuanguka ndani ya shimo maeneo ya Kasagam jioni ya Jumatatu.

Punde baada ya ajali hiyo kutokea maafisa wa usalama walikimbia kwenye eneo la tukio na kufurusha kikundi cha watu kilichokuwa kimejumuika pale.

Kulingana na kamanda wa kaunti Samuel Anampiu, lori hilo lilikuwa linatoka Kondele kuelekea Ahero ajali hiyo ilipotokea mwendo wa saa moja unusu.

Dereva wa lori hilo ambaye hajulikana alipoa alitoweka punde baada ya ajali kutokea. Juhudi za kumtafuta zimeanza. 

Lori hilo linadaiwa kupoteza mwelekeo lilipokuwa linapiga kona.

Mapema siku hiyo, kinara wa ODM Raila Amolo Odinga alisihi Wakenya kujifunza kutokana na tukio la mlipuko wa tangi ambalo lilsababisha maafa ya watu 13 na kujeruhi wengine 31 usiku wa Jumamosi maeneo wa Gem.

 Raila alisema kuwa anatumai kuwa hilo litakuwa tukio la mwisho ambapo Wakenya watang'angana kuchota mafuta baada ya lori kuanguka.

Aliwaomba Wakenya kutoroka kutoka kwenye eneo la tukio iwapo wakati wowote ajali ianyohusisha lori la mafuta inajitokeza.

Taasisi ya mafuta Afrika Mashariki (PIEA)  ilitoa ombi kwa wale ambao waliweza kuchota mafuta maeneo ya Malalanga kabla ya mlipuko kuyarejesha kwa maafisa wa usalama  walio  karibu nao kwani ni hatari  sana kuyameka ndani ya nyumba.

Kulingana na PIEA, mafuta huhifadhiwa kwa chombo maalumu ila sio kwa vibuyu na vyombo vingine ambavyo wanakijiji walitumia kuteka.