Biblia inasema, sema ukweli, ukweli wangu naomba kazi - Justina amwambia Ruto

Alidhibitisha kwamba bosi wake Wajackoyah alimfukuza chamani Roots.

Muhtasari

• Wamae pia alisema kitendo cha Wajackoyah kutangaza amejiunga na upinzani ni ishara kuwa alikuwa mradi.

Justina Wamae amuomba Ruto kazi katika serikali yake.
Justina Wamae amuomba Ruto kazi katika serikali yake.
Image: Twitter

Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais kupitia chama cha Roots, Justina Wamae amempongeza rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kwa ushindi wao kuidhinishwa na mahakama ya upeo.

Wamae ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa na mvurugano na kiongozi wa chama chake George Wajackoyah aliwapongeza wawili hao huku pia akidokeza kwamba anataka kazi.

Alinukuu biblia kwamba inasema ukweli ni muhimu na yeye akasema ukweli wake ni kwamba anaomba kazi kutoka serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Ruto.

“Justina Wamae amenyenyekea, asante Mheshimiwa Rais William Ruto na Rigathi Gachagua. Biblia inasema, sema ukweli, ukweli wangu naomba kazi. Niko tayari kutumikia,” Wamae aliandika kwenye Twitter yake.

Awali alionekana kumkejeli aliyekuwa kiongozi wa chama chake Roots, Wajackoyah baada ya wakili huyo kusema kwamba yeye ni rasmi mwanachama wa upinzani.

Wamae alisema maneno hayo ya Wajackoyah yalionesha wazi kwamba pia yeye alikuwa anatafuta kazi na imedhibitisha alikuwa mradi wa mrengo wa upinzani.

“Kwa taarifa yako Bosi alinifukuza na leo ametangaza ako UPINZANI. Lakini ni dhibitisho kwamba alikuwa mradi.....pia yeye ALIKUWA anatafuta kazi ila ubashiri wake umeungua,” Wamae alikejeli hatua ya Wajackoyah kutangaza kwamba amejiunga upinzani rasmi.

Hii si mara ya kwanza mwanasiasa huyo kutangaza kwamba anaomba kazi katika serikali ya William Ruto kwani wakati IEBC ilimtangaza kuwa rais mteule, Wamae alikuwa mstari wa mbele kutuma pongezi zake na kuomba kazi, jambo ambalo lilizidisha kutokota kwa mgogoro kati yake na Wajackoyah kwa kile uongozi wa chama ulisema ni kuenda kinyume na kanuni za chama.