Mwalimu wa kike aeleza sababu ya kukubali kuolewa na mwanafunzi aliyemfunza sekondari

"Baada ya kusisitiza nia yake kwangu, kitu Fulani kilibadilika ndani yangu, nilijipata nimempenda na kutaka kumuona kila wakati,” mwalimu huyo alisimulia.

Muhtasari

• Kwa upande wake, Jeannette alisema kwamba ungamo hilo la mwanafunzi wake kuwa anampenda lilikuwa la mshangao wa aina yake.

• Hakuwa anaamini kwenye masikio yake kwamba mwanafunzi wake alikuwa anaumwaya moyo wake kwake kuhusu mapenzi.

Mwalimu aolewa na mwanafunzi wake
Mwalimu aolewa na mwanafunzi wake
Image: Screengrab//Afrimax English

Mwalimu mmoja wa kike kutoka taifa la DRC amesimulia kwa undani sababu zilizomfanya kukubali posa ya mvulana aliyemfunza shule ya sekondari na kuolewa naye licha ya utofauti mkubwa wa umri baina yao.

Kwa mujibu wa Jeannette, alikubali kuwa mke wa Hassan Mamba Remy ambaye alikuwa mwanafunzi wake katika shule ya sekondari na kusema kwamba hajutii kufanya uamuzi huo ulioacha jamii vinywa wazi.

“Ndio vile mlisikia ni kweli, mimi nilikuwa mwalimu na bwanagu alikuwa mwanafunzi wangu. Sasa tuna miaka 5 katika ndoa yetu,” Jeannette alisema.

 Kwa upande wake, Remy alisimulia jinsi alijpata kuwa na ujasiri wa kumtongoza mwalimu wake.

Alisema;

“Tumekuwa kwa ndoa kwa miaka 5 na tumebarikiwa na watoto wawili. Mke wangu alikuwa ni mwalimu wangu. Alikuwa na mazoea ya kuja nyumbani kunisaidia kwa masomo ya ziada, hii inamaanisha tulitumia muda mwingi pamoja. Na pole pole, nilijipata nimeanza kumpenda na darasani akifunza sikuwa natilia maanani masomo kwani nilikuwa namuwaza muda wote.”

Licha ya mwalimu wake kumuacha kwa pengo la miaka 12, Remy hakufa moyo wala kujali jamii itamchukulia kivipi.

“Katika mwaka wa mwisho mitihani ilipokuwa inakaribia, niliamua kuweka wazi hisia zangu kwake, nilimwambia jinsi nilimpenda na jinsi nilivyokuwa nikishindwa kumwambia kwa vile ananishinda umri. Hakusema hapana, aliniambia nimpe muda afikirie,” alisema.

Kwa upande wake, Jeannette alisema kwamba ungamo hilo la mwanafunzi wake kuwa anampenda lilikuwa la mshangao wa aina yake.

Hakuwa anaamini kwenye masikio yake kwamba mwanafunzi wake alikuwa anaumwaya moyo wake kwake kuhusu mapenzi.

“Nilikuwa namuona darasani kwamba hakuwa anamakinika katika masomo. Mara ya kwanza nilifikiria alikuwa ananifanyia mzaha, hata nikamjibu kwa jeuri kwamba alikuwa ananikosea heshima. Lakini unajua hatima ya mtu haijulikani, aghalabu watu wenye tunapuuza ndio wanakuja kuwa wa maana kwetu. Baada ya kusisitiza nia yake kwangu, kitu Fulani kilibadilika ndani yangu, nilijipata nimempenda na kutaka kumuona kila wakati,” mwalimu huyo alisimulia.

Hata baada ya kupendana, vizingiti vingi vilitokea kutoka kila upande, watu wa ukoo wa Remy wakimtaka kukomesha uhusiano huo kwani walimuona mwalimu kama rika la mama yake.

Lakini penzi lao halikufa na miaka 5 baadae, wanajivunia familia yao na watoto 2.