SIASA ZA TANGATANGA

Kuria aondoa mgombeaji wake kwenye kinyang'anyiro cha Kiambaa

Moses Kuria alieleza kuwa uamuzi ulifikiwa baada ya kujadiliana na Ruto, kufurahisha wenzake na kwa umoja wa 'mahustler

Muhtasari

•Moses Kuria alieleza kuwa uamuzi ulifikiwa  baada ya kujadiliana na Ruto, kufurahisha wenzake na kwa umoja wa 'mahustler

•Chama cha PEP kilikuwa kimemteua Raymond Kuria kama mgombeaji wake

Mgombeaji Raymond Kuria wa PEP
Mgombeaji Raymond Kuria wa PEP
Image: Hisani

Chama cha People’s Empowerment Party(PEP) kinachoongozwa na Moses Kuria kimemuondoa mgombeaji wake kwenye uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Kiambaa, Raymond Kuria.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Facebook, mbunge wa Gatundu Kusini alitangaza kuwa uamuzi huo baada ya kukutana na kujadiliana na naibu rais William Ruto.

“Tulijadiliana na mkubwa wangu mtukufu naibu rais William Ruto jana kuhusiana na jambo hili. Ili kuwafanya wenzangu wafurahie na kwa umoja wa muungano wa mahasla, chama cha PEP hakitateua mgombeaji kwenye uchaguzi wa Kiambaa” Kuria alisema.

ujumbe wa moses kuria
ujumbe wa moses kuria
Image: Hisani

Kuria alieleza kuwa uamuzi wa chama cha PEP kuteua mgombeaji haukuchukuliwa vizuri  na baadhi ya wenzake wa Tangatanga huku akitaja haswa Rigathi Gachagua wa Mathira na Kimani Ichungwa wa Kikuyu. Kuria alikuwa amekashifiwa sana kwani chama cha UDA ambacho pia kinahusishwa na naibu rais kilikuwa kimeteua John Njuguna kama mgombeaji wake.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani mkuu wa naibu rais alimuomba msamaha Raymond Kuria ambaye alikuwa ashatangazwa kwamba angewania kiti na tikiti ya chama hiyo, watu wa Kiambaa na wanachama wa chama cha PEP akidai kuwa wangesitikishwa na tangazo hilo.

Kuria alisisitiza kuwa nia ya chama cha PEP ilikuwa kuwapa ujumbe wa matumaini na uzinduo mpya wakazi wa Kiambaa. Alisema kuwa chama hicho kinaongozwa na watu wa kawaida haswa vijana ilhali chama cha UDA kinaongozwa na wabunge walio madarakani.