UKULIMA WA MIWA

Nzoia: Wakulima wa miwa walalamika kutolipwa zaidi ya Sh700M

Wakulima upande wa Nzoia wametishia kuandamana kuelekea kiwanda cha kutengenezea sukari cha Nzoia wakilalamikia kutopokea malipo yao

Muhtasari

•Kiongozi wa wakulima upande huo, Jack Munialo amemkashifu mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho huku akisema kuwa alivunja ahadi aliyompatia mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi kuwa wakulima wangepokea malipo yao baada ya wiki moja.

SHAMBA LA MIWA
SHAMBA LA MIWA
Image: Hisani

Wakulima wa miwa upande wa Bungoma wametishia kuandamana kuelekea kiwanda cha kutengenezea sukari cha Nzoia wakilalamikia kutopokea malipo ya zaidi ya milioni mia saba.

Wakulima hao wametangaza kuwa wataandama na hadi kiwandani hicho siku ya Jumatatu  wiki ijayo iwapo hawatakuwa wamepokea malipo yao bado.

Kiongozi wa wakulima upande huo, Jack Munialo amemkashifu mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho huku akisema kuwa alivunja ahadi aliyompatia mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi kuwa wakulima wangepokea malipo yao baada ya wiki moja.

Sisi wakulima wa Nzoia tumegundua kuwa tusipofanya maandamano  hawezi lipa pesa, anatembea na pesa kwa gari kama mchawi. Ningependa kuwaagiza wakulima wote wa Nzoia, kwa kuwa watoto wanakuja likizo fupi, Jumatatu saa mbili tukutane kwa lango la Nzoia Sugar Company. MD akipe pesa!”  Munialo alisema.

Munialo pia alitoa ombi kwa mbunge Wafula Wamunyinyi, mwenyekiti wa muungano wa NOCCO Christopher Sifuna na wakurugenzi wote wa NOCCO kuhudhuria maandamano hayo.

Tangazo hili linajiri huku baadhi ya wakulima wakishinikiza kuwepo maandamano ya mara kwa mara kwani hiyo ndiyo njia pekee wanaweza dai malipo yao.  Mmoja wa wakulima hao amekashifu mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Michael Wanjala kwa kupuuza kilio cha wakulima.

Mkurugenzi Mkuu wa Nzoia sugar Co. Michael Wanjala
Mkurugenzi Mkuu wa Nzoia sugar Co. Michael Wanjala
Image: HISANI

“Tulipoitisha maandamano, MD wa Nzoia alisema kuwa atakuwa amelipa deni yetu ya milioni mia tano kwa  kipindi cha siku thelathini, saai deni imefika milioni mia saba. Tunataka pesa yetu kwa sababu tunaskia MD anataka kutoroka” Kibet alisema.

Kibet aliwaagiza wakulima kusimamisha shughuli ya kukata miwa huku akiwaambia kuwa tingatinga za kubeba miwa ile hazitaruhusiwa kubeba.

Munialo alimpongeza Wamunyinyi kwa kuwatetea wakulima wa miwa katika kiwanda cha Nzoia na kuwaomba viongozi wengine kutoka eneo hilo kuungana na wakulima ili kutetea haki yao.