Sharti Jubilee ishinde Kiambaa! Ngunjiri asema kampeni za Kiambaa ni muhimu kuliko majadiliano na ODM

Amesema kuwa iwapo Jubilee haitapata ushindi itakuwa ngumu kuunda muungano na vyama vingine

Muhtasari

•Mwanasiasa huyo wa mrengo wa Kieleweke amesema kuwa ushindi katika chaguzi hizo ni muhimu sana kwa sasa kuliko majadiliano ya kuunda muungano na chama cha ODM ambayo yanaendelea.

•Hivi majuzi mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ambaye anaunga mkono mgombeaji wa UDA alkashifu chama cha Jubilee kwa kile alisema ni kuiga mitindo ya kampeni ya chama cha UDA.

Mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu
Mbunge wa Nyeri, Ngunjiri Wambugu
Image: The Star

Mbunge wa Nyeri Ngunjiri Wambugu ameapa kuwa ni sharti chama cha Jubilee kitwae ushindi katika chaguzi ndogo za eneo bunge la Kiambaa na wadi ya Muguga mwezi ujao.

Mwanasiasa huyo wa mrengo wa Kieleweke amesema kuwa ushindi katika chaguzi hizo ni muhimu sana kwa sasa kuliko majadiliano ya kuunda muungano na chama cha ODM ambayo yanaendelea.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Ngunjiri alisema kuwa viongozi wenye nia ya kuendeleza chama wamepea kipaumbele kampeni za Kiambaa.

"Cha muhimu zaidi kwa sasa ni kutwaa ushindi katika chaguzi ndogo za Kiambaa na Muguga. Tukipata ushindi basi tutaweza kuwa na majadiliano ya kuunda muungano kwani chama chochote kingependa kushiriki majadiliano nasi kwa msingi wa kuwa Jubilee ndicho chama kinachotawala eneo la mlima Kenya" Ngunjiri alisema.

Mbunge huyo alisihi maafisa wa chama cha Jubilee ambao wanaendeleza mazungumzo ya kuunda muungano kuangazia ushindi wa chaguzi ndogo hizo kwanza.

"Iwapo tutapoteza kwenye uchaguzi wa Kiambaa, itakuwa ngumu kuwa na majadiliano ya kuunda muungano na vyama vingine kwa vyama hivyo vitasema kuwa chama chetu hakina uwezo" Ngunjiri aliendelea kusema.

Ngunjiri lieleza imani yake kuwa Jubilee itakuwa kwenye serikali ambayo itatawala muhula ujao. Alisema kuwa chama hicho kitakubali majadiliano na chama chochote kingine ambacho kingependa kuunda serikali itakayofuata.

Alisema kuwa ushindi wa Kiambaa na Muguga utasaidia chama cha Jubilee kujikomboa

Shughuli za kampeni katika eneo bunge la Kiambaa zimeendelea kunoga huku wanasiasa wa chama cha Jubilee na kile cha UDA wakijitosa uwanjani kuwasihi wakazi kupigia kura mgombeaji wao.

Bendera ya Jubilee inapeperushwa na Kariri Njama huku John Njuguna Wanjiku akipeperusha bendera ya UDA.

Siku chache zilizopita , mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ambaye anaunga mkono mgombeaji wa UDA alkashifu chama cha Jubilee kwa kile alisema ni kuiga mitindo ya kampeni ya chama cha UDA.

Kuria alikashifu wanasiasa wa chama hicho wakiongozwa na gavana wa Kiambu James Nyoro kwa kuiga kitendo cha UDA cha kununua bidhaa kutoka kwa wauza mboga sokoni maeneo ya Kiambaa.

"Marehemu Jubilee wanaiga hafla za ununuzi za mrengo wa Hustler. Wizi ni ni mfumo wa udanganyifu. Karibu kwa mrengo wa Hustler gavana James Nyoro." Kuria alisema.

Hata hivyo, Ngunjiri amesema kuwa wanasiasa ambao walihamia chama cha UDA watakaribishwa kujadiliana na chama cha Jubilee iwapo watataka.