Wakenya wanaoishi Uswizi kufurahia huduma za ubalozi

Muhtasari

• Balozi Andrew Kihuran alisema mataifa haya mawili yamekuwa na ushirikiano thabiti katika sekta ya utalii na biashara nyinginezo.

• Mauzo ya Kenya ni shilingi bilioni 4.8 ilhali uagizaji kutoka Uswizi ukiwa wa thamani ya shilingi bilioni 8 kila mwaka.

• Uagizaji wa Kenya kutoka Uswizi ni dawa za kumaliza magugu, dawa za kuua kuvu, kemikali, rangi, mashine pamoja na vifaa vya matibabu.

Balozi Andrew Kihuran
Balozi Andrew Kihuran
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufungua ubalozi mpya Jijini Bern nchini Uswizi kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Uswizi.

Akizungumza kabla ya ziara rasmi ya Rais Kenyatta nchini Uswizi, Balozi Andrew Kihuran alisema kufunguliwa kwa ubalozi huo mpya kutasaidia kuboresha biashara za pande mbili ambazo zimekuwa zikiongezeka, mauzo ya Kenya yakiwa ya thamani ya shilingi bilioni 4.8 ilhali uagizaji kutoka Uswizi ukiwa wa thamani ya shilingi bilioni 8 kila mwaka.

“Suala lingine la kimsingi tunalojishughulisha nalo ni kuendeleza biashara. Mnaweza kufahamu kwamba kuna biashara nyingi kati ya mataifa haya mawili. Kenya ni mshirika mkuu wa kibiashara na nchi ya Uswizi kwa kuwa katika nafasi ya 16 Barani Afrika,” kasema Balozi Kihuran.

Balozi huyo wa Kenya alisema licha ya biashara hizo kunufaisha zaidi Uswizi, Kenya imeendelea kuongeza biashara zake za kahawa, majani chai, mboga na matunda.

Aliongeza kwamba biashara za pande mbili mwaka 2021 zilikuwa kubwa huku Kenya ikiwa kitovu kikuu cha maua kwa Uswizi.

Uagizaji wa Kenya kutoka Uswizi ni dawa za kumaliza magugu, dawa za kuua kuvu, kemikali, rangi, mashine pamoja na vifaa vya matibabu.

“Kwa hivyo, majukumu yetu ni kuweza kuona jinsi ya kuimarisha biashara hizo kati ya mataifa haya mawili. Sio tu kwa misingi ya kiwango cha biashara bali pia upana, ili kuhakikisha ni bidhaa gani zingine tofauti zinaweza kuuzwa kati ya mataifa haya mawili,” kasema.

Aidha, Balozi Kihuran alisema mataifa haya mawili yamekuwa na ushirikiano thabiti katika sekta ya utalii, huku akiongezea kwamba Kenya ilikuwa ikipokea zaidi ya watalii 9,000 kila mwaka kutoka nchini Uswizi kabla ya kutokea kwa janga la Covid-19.

Alieleza matumaini kwamba mchakato unaoendelea wa kutoa chanjo dhidi ya Covid-19 utafufua sekta ya utalii huku Kenya ikisajili ongezeko la idadi ya watalii kutoka nchini Uswizi.

“Uswizi imetoa chanjo kwa tariban asilimia 70 ya raia wake na bila shaka nchini Kenya tunaendelea kuimarisha kiwango cha utoaji wa chanjo. Tunatarajia kiwango cha watalii kuanza kukua tena na ni wajibu wa ubalozi huu kuimarisha ukuaji wa biashara hizo za utalii,” kasema Balozi Kihuran.

Aidha, Balozi huyo wa Kenya nchini Uswizi alisema Rais Kenyatta atazuru Jiji la Geneva ambapo anatazamiwa kuhutubia Kongamano la Afya Ulimwenguni tarehe 22 Mwezi Mei.

Alisema hotuba ya Rais katika Kongamano la Afya Ulimwenguni itaangazia jinsi ambavyo Kenya imekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe masuala ya afya ulimwenguni.

“Mkutano huo wa Geneva ni Kongamano la Ulimwengu kuhusu Afya ambalo huandaliwa kila baada ya mwaka. Na mkutano huo hususan kwa wakati huu utahutubiwa na Mheshimiwa Rais.

“Hii itakuwa mara yake ya kwanza kuhutubia kongamano hili. Ni muhimu kwa sababu inaonyesha jinsi ambavyo Kenya inaunga mkono masuala yatakayojadiliwa na kongamano hili kuhusu afya,” kasema.

Kongamano hilo la 75 la Afya Ulimwenguni litaanza kwa kipindi cha hadhi ya juu tarehe 22 Mei kukiwa na hotuba za Rais aliyechaguliwa wa Kongamano la Afya, Viongozi wa Nchi, wageni mashuhuri na hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la WHO pamoja na maonyesho ya Tuzo za Mkurugenzi Mkuu za Afya.  

Maudhui ya mwaka huu ya Kongamano la Afya Ulimwenguni ni "Afya kwa Amani, Amani kwa Afya".