Majaji waliokataliwa na Uhuru hatimaye waapishwa na Ruto

Majaji hao walikuwa miongoni mwa wengine 40 walioteuliwa na JSC mwaka 2019 baada ya zoezi kali la kuhakikiwa

Muhtasari

• Ruto aliahidi kuheshimu uhuru wa idara ya mahakama.

• Alisema atafanikisha mazungumzo ya kila mara kila wakati kuna jambo kati ya idara husika.

Rais wa tano Ruto na baadhi ya ahadi zake siku ya kuapishwa
Rais wa tano Ruto na baadhi ya ahadi zake siku ya kuapishwa
Image: Facebook//William Ruto

Majaji sita ambao walikuwa wameteuliwa na tume ya huduma kwa mahakama (JSC) mwaka 2019 na majina yao kukataliwa na rais mustaafu Uhuru Kenyatta, hatimaye wameapishwa.  

Majaji hao ni Weldon Korir, George Odunga, Aggrey Muchelule na Joel Ngugi wa mahakama ya rufaa na Evans Makori na Judith Omange wa Mahakama ya Mazingira na ardhi. 

Kuapishwa kwa majaji hao kunajiri siku moja tu baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na rais William Ruto.

Ruto alichapisha majina ya majaji hao kwenye gazeti rasmi la serikali muda mfupi tu baada ya kuapishwa kuwa rais wa Kenya.  

Akiwahutubia majaji hao rais Ruto aliahidi kuheshimu uhuru wa idara ya mahakama. Alisema atafanikisha mazungumzo ya kila mara kila wakati kuna jambo kati ya idara husika.

Rais alisema lazima kama serikali wakabiliane na ukiukaji wa sheria na kutoa wito kwa wakenya kufahamu kuwa kila mtu anaongozwa na sheria na katika sheria hakuna mapendeleo. 

“Hata mimi kama rais nina kimo changu katika sheria na siwezi fanya jambo nje ya sheria, kila mmoja wetu anafaa kufuata sheria,” Ruto alisema.  

Majaji hao walikuwa miongoni mwa wengine 40 walioteuliwa mwaka 2019 baada ya zoezi kali la kuhakikiwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kati ya Julai na Agosti mwaka huo. 

Mnamo Juni 2021, Uhuru aliteua majaji 34 lakini akawaacha nje majaji sita akitaja masuala ya uadilifu.

Mnamo Oktoba 2021 punde tu baada ya Mahakama Kuu kuamuru Uhuru kuteua majaji waliosalia ndani ya siku 14, Kariuki alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.