Watoto wawili kati ya 4 waliopewa sumu na baba yao huko Homa Bay wafariki

Mtoto mmoja alifariki akiwa ICU huku mwingine akifariki akipokea matibabu kwenye wadi ya kawaida

Muhtasari

• Maafisa hao walisema watoto wengine wawili bado wako katika mbaya na  wanapokea matibabu katika hospitali hiyo.

Image: Star

Watoto wawili kati ya wanne waliopewa sumu na kudungwa kisu na baba yao Jumanne usiku huko Homa Bay wamefariki wakipokea matibabu.

Ndugu hao mapacha wenye umri wa miaka 3 walifariki kutokana na majeraha waliyopata baada ya kudungwa kisu tumboni na baba yao. Walifariki Alhamisi asubuhi.

Daktari Charles Ocholla alisema mapacha hao walikuwa na matatizo mara mbili majeraha ya kisu na na sumu waliopewa ambayo ilikuwa imeathiriubongo na viungo vingine vya ndani ya mwili.

Daktari alisema kuwa kemikali inayojulikana kama Oganophosphate iliingia katika viungo vya ndani vya mwili.

"Kemikali hiyo illifika kwenye ubongo na matumbo ya watoto. Walichanganyikiwa na kutapika kupita kiasi,” Ocholla alisema.

"Walishughulikiwa na madaktari wenye uwezo na wataalam lakini kwa bahati mbaya walifariki,” daktari  alisema.

Maafisa wa matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti hiyo walisema mtoto mmoja alifariki katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) huku kakake akifariki akipokea matibabu katika wadi ya kawaida.

Maafisa hao walisema watoto wengine wawili bado wako katika mbaya na  wanapokea matibabu katika hospitali hiyo.

Watoto hao walilazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya baada ya kupewa sumu na kudungwa kisu na baba yao aliyejiua baadaye kwa kunywa sumu eneo la East Kochia, kaunti ya Homa Bay. Watoto hao walikuwa wenye umri wa kati ya miaka 3 na 9.

Mama yao Monica Atieno Ndeda, ambaye hakuwa nyumbani wakati wa tukio, alitoa wito kwa wasamalia wema kumsaidia kuwazika walifariki.

 

Ndeda alisema pia hana uwezo wa kulipa bili ya hospitali ambayo ni ada ya upasuaji, ICU na chumba cha kuhifadhi maiti.

"Sina pesa za kulipia bili za hospitali na kushughulikia mazishi ya familia yangu. Niko peke yangu na ninahitaji kusaidiwa,” Ndenda alisema.