Mama Ngina ampigia debe Raila ashauri Mt Kenya kumsikiliza Uhuru

Muhtasari

• Mama Ngina Kenyatta amewataka watu kumuunga kinara wa vuguvugu la Azimio la Umoja Raila Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Raila Odinga (Facebook)

Mama Ngina Kenyatta, mke wa rais wa kwanza wa taifa la Kenya na ambaye ni mamake rais wa sasa Uhuru Kenyatta amewataka wakenya wote kufuata kile ambacho rais Uhuru Kenyatta anawaelekeza – Kuunga kinara wa ODM Raila Odinga mkono katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akizungumza kwa lugha ya kikuyu katika hafla ya mazishi siku ya Jumanne katika eneo bunge la Gatundu ya Kusini, Mama Ngina aliwahakikishia wakaazi kwamba rais Kenyatta ambaye ni mwanawe hawezi kuwapotosha kwa kuwataka wamuunge Raila mkono.

“Kiongozi wako hawezi kukupotosha au kukuonyesha njia mbaya ya kufuata,” Mama Ngina alisema.

Pia kwa wale wanaoelewa lugha hiyo walitafsiri maneno yake kwamba aliwataka watu waungane ili kudumisha umoja wa kitaifa na kufuata rais Kenyatta. 

Aliongeza kuwa hawana muda kuwasikiliza  wenye matusi midomoni mwao, kauli hii ikionekana kumlenga naibu rais William Ruto na wafuasi wake.

Kwa kile kinasemekana kwamba alidokeza kulikuwepo na sababu kubwa ya mwanawe kuvunja uswahiba na naibu rais, Mama Ngina alisema kwamba Uhuru alikuwa na sababu kukatisha uhusiano wake wa kisiasa na Ruto, akisema kuwa naibu wake alikuwa na matatizo mengi.

Ikumbukwe mwezi mmoja uliopita katika Ikulu ndogo ya Sagana, rais Uhuru alikutana na wakaazi pamoja na viongozi kutoka mlima Kenya ambapo alitangaza rasmi kumuunga mkono Raila katika mkutano huo uliopewa jina Sagana 3.

Wengi wanahisi hatua ya Mama Ngina kuwataka wenyeji wa Mlima Kenya kumuunga mkono Raila ni mwanzo wa kuporomoka kwa Ruto kutoka kilele cha Mlima Kenya, huku baadhi wakisema kwamba kwa jumla familia ya Kenyatta pekee ndiyo inayounga mkono mgombea urais wa vuguvugu la Azimio.

Mgawanyiko huu mkubwa baina ya viongozi na wakaazi wa eneo hilo lenye wingi wa kura unazidi kila uchao huku baadhi ya viongozi wakiibua masuala ya kihistoria kuhusu kiapo ambacho jamii za Mlimani zilikula Yamini kutozikiuka.